Monday, February 22, 2010

UINGEREZA KUWABANA WANAFUNZI WA KIGENI

Sheria kali zilizoanzishwa nchini Uingereza kuhusu wanafunzi kutoka nje ya ulaya wanaokuja nchini humo kwa masomo zitawafanya wanafunzi wengi kutoka barani Afrika kutoweza kusomea Uingereza.

Idara ya uhamiaji Uingereza - UK Border Agency, imesema watu wengi wametumia vibaya na kukiuka sheria za uombaji wa viza hasa za wanafunzi.

Serikali ya Uingereza imeongezea vikwazo kupiga vita ukiukaji wa sheria hizi. Ukiukaji wa sheria umekuwa ukifanyika kufuatia kukomeshwa kwa uchunguzi uliokuwa ukifanywa kuhakikisha kwamba wanafunzi wanarudi nchini mwao baada ya kumaliza masomo yao na mda waliopewa na idara ya uhamiaji Uingereza kumalizika.

Ingawaje wanafunzi wanachunguzwa kabla ya kupewa viza, hawajakuwa wakichunguza hivi karibuni kuhakikisha kwamba wamerudi nchini mwao.Imekuwa vigumu kujua idadi ya wale wanaorudi na wale wanaoishi Uingerza kinyume cha sheria. Idara ya uhamiaji inasema kwamba itakuwa vigumu sana kuvunja sheria za uhamiaji siku zijazo. Mnamo mwaka 2011, Idara hio itakuwa na technolojia ya kipekee duniani kuwachunguza watu wakiingia na kutoka Uingereza.

Idara hii imeanzisha vikwazo mbalimbali ambavyo wanafunzi wengi kutoka nchi za kigeni wanasema ni vikali mno. Mwaka uliopita mwezi Machi, Idara ya uhamiaji ilibadilisha taratibu ambazo wanafunzi kutoka nchi zingine hutumia kuomba viza za kuja Uingereza na kuanzisha mfumo ujulikanao kama Tier 4 Points based system.

Katika mfumo huu, vyuo vyote vya elimu ya juu ni lazima vijiandikishe katika idara ya uhamiaji. Vikitimiza mahitaji yote, vitapewa leseni ya kuwaleta wanafunzi kutoka nchi mbalimbali hapa Uingereza. Wanafunzi nao wanahitajiwa kuwa na pointi arubaini ndio watapewa viza. Wanafunzi watashinda pointi thelathini wakipewa barua ya kuomba viza kutoka chuo ambacho kimesajiliwa. Watashinda pointi kumi kama watakuwa na karo yote na pesa za matumizi za mwaka mmoja.

Wakitaka kuongezea mda wa viza zao wakiwa Uingereza, watahitajiwa kuonyesha kwamba wamekuwa na kiasi cha pauni 800 kila mwezi, kama chuo chao kiko mjini London na pauni 600 kila mwezi kama chuo chao kiko nje ya mji wa London.

Kabla ya kuongezewa mda wao kama wanafunzi, wale wanaoishi mjini London watahitajika kuonyesha kwamba kiasi cha £ 1600 kimekuwepo kwenye akaunti yao ya benki kwa mda wa siku 28. Wale wanaoishi nje ya mji wa London, watatakiwa kuonyesha wamekuwa na kiasi cha £ 1200 kwenye akaunti yao ya benki kwa mda wa siku 28.

Wanafunzi watakaopewa fursa kufanya kozi za muda mfupi wataruhusiwa kufanya kazi kwa masaa kumi kila wiki lakini kama wanasomea shahada, wataruhusiwa kufanya kazi masaa 20.

Wanaopinga hatua hii wanasema vikwazo hivi havijafanikiwa. Dr. Zakir Hussein, mkuu wa chuo cha London Trinity , anasema hivi vikwazo vimefanya wanafunzi wengi kuja Uingereza wakiwa hawawezi kuzungumza Kiingereza, wengi wao wakitoka bara la Asia.

Idara ya uhamiaji Uingereza imesimamisha kwa muda uombaji wa viza kutoka kaskazini mwa India, Nepal na Bangladeshi. Walichukua hatua hii kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi walioomba viza eneo hilo kutoka 2,000 mwaka 2008 hadi 13,500 mwaka uliopita. Mabadiliko haya yatawaathiri vibaya wenye vyuo ambavyo havitoi shahada.

Jeremy Oppenheim ambaye ni mkuu wa mfumo wa Tier 4 Point based amesema kwamba kuanzia mwezi Machi mwaka huu, idara ya uhamiaji itawapa viza wanafunzi watakaopata nafasi kwenye vyuo ambavyo vitatoa shahada na zaidi . Mfumo huu utamaliza mafunzo yote ambayo wanafunzi hawatapewa shahada.

David Game, mkuu wa muungano wa vyuo wa David Game group of colleges, amesema kama serikali ya Uingereza itafuata sera hii kwa makini, basi utakuwa mwisho wa vyuo kama vyake. Kama idara ya uhamiaji itachukua hatua hiyo, David anasema yeye ataacha nchi yake na kuanzisha vyuo vya elimu ya juu nchi zingine.


No comments:

Post a Comment