Tuesday, February 2, 2010

TATIZO LA UMEME ZANZIBAR KUMALIZIKA HIVI KARIBUNI

Tatizo la ukosekanaji wa umeme Zanzibar linatarajiwa kumalizika ndani ya wiki tatu, kampuni ya umeme Zanzibar ilisema.

"Tunaendelea vizuri na kazi ya kurejesha umeme, kikosi cha mafundi kutoka Uingereza, Afrika Kusini, Zanzibar, na kampuni ya Ericson wamekua wakifanya kazi kwa bidii na tunatarajia umeme utarejea mnamo Febuari 20 mwaka huu, kaimu meneja ZECO" Bw. Hassan Mbarouk alisema.

Nae Ofisa Uhusiano wa ZECO alisema Bw. Salum Abdallah alisema kua Mafundi wanatarajiwa kuhamia Ras Kiromoni huko Dar-es-Salaam kwa ajili ya kwenda kufunga baadhi ya vifaa.

"Bado tunawaomba Wazanzibari kuwa wastahamilivu wakati tukiwa tunamalizia kazi hii.Tunatarajia Serikali itafanikiwa mpango wake wa kununua majenereta ya akiba" alisema.

Hata hivyo chanzo kutoka Wizara ya Maji Ujenzi Nishati na Ardhi kimesema Serikali ilitarajia kuingia mkataba na kampuni ya Katapila kwa kuleta majenereta yenye nguvu za megawatts 25.

Waziri kiongozi Mh. Shamsi Vuai Nahodha alisema wiki iliopita kwamba Serikali imeziomba nchi washirika wa maendeleo kusaidia ununuzi wa majenereta ya akiba ikiwa ni katika jitihada za kuleta umeme.

Wakati Wazanzibari wakikabiliwa na tatizo la maji na biashara kutokana na kukosekana umeme, ZECO imesema katika kipindi ambacho hakukuwa na umeme kisiwani humo, imepoteza Sh bilioni nne na Wizara ya Fedha na Uchumi imepoteza asilimia 30 ya mapato yake.

Tangu Desemba 10, mwaka huu kisiwa cha Unguja kimekosa umeme baada ya kifaa kimoja kilichopo katika kituo cha umeme cha Fumba kuharibika na kusababisha kutofanya kazi kwa waya wa kupitisha umeme wa chini ya bahari wa megawati 45 kutoka gridi ya Taifa kupitia Ras Kiromoni hadi Zanzibar.

Kwa mujibu wa Nahodha, Marekani kupitia Shirika lake la Millennium Challenge Corporation (MCC), imekubali kufadhili uwekaji wa waya huo wa megawati 100. Mradi huo utagharimu dola za Marekani zaidi ya milioni 63 ambapo tayari zabuni zimeshatangazwa na unatarajiwa kukamilika mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment