Thursday, February 18, 2010

MUAFAKA - ZANZIBAR

Naikumbuka hadithi ya mzee Haji. Alikuwa mzee wakujipenda sana, akivaa nadhifu kabisa, Kanzu, kofia, koti na makbadhi ilikuwa kawaida yake, Akipenda sana kula hasa pilau na biriyani. Shughuli yake kubwa ilikuwa kutegeya nje ya sehemu za kukodisha masufuria, sahani, majamvi n.k.

Liondokapo rikwama na mizigo hiyo basi yeye hujifanya mmoja wa washindikizaji wa mzigo. Wanapofika penye shughuli hujifanya bizi katika matayarisho. Atatandika majamvi na kujifanya kama mmoja ya wahusika, almuradi aondoke hapo kashiba, hii ilikuwa kawaida yake ya kila siku.

Siku mmoja likaondoka rikwama limejaza majamvi. Mzee Haji akaliandama, bizi kusukuma. Kilima cha kwerekwe kapandisha na nyimbo za hamasa kuimba, Safari iliishiya Fuoni, mzee Haji
taabani kwa uchofu.

Majamvi yakashushwa. Mzee Haji akashiriki kikamilifu hata kutandika akijuwa ya kuwa biriyani iko njiani. Mara yakaletwa magunia ya karafuu, Mzee Haji kashangaa. Viiipi hapa? Zikaanza kutandazwa karafuu majamvini, mzee Haji kakosa subra, matusi jujuu. Analaumu-kwa nini asiambiwe mapema.

Maridhiano Zanzibar ilikuwa bashraf tu. Nyimbo hasa wameiimba Dodoma. Serikali shirikishi baada ya uchaguzi, kura za maoni baada ya uchaguzi, sasa sijui baina ya uchaguzi na kura za maoni itakuwepo serikali ipi? na hasa lakujiuliza ni hiyo kura ya maoni ni lini? Labda September 2015. Laa-haulla! Sijui CUF itakula biriyani au tuta anika karafuu.
Mwenye Enzi Mungu atusaidie.

No comments:

Post a Comment