Thursday, February 18, 2010

GIZA ZANZIBAR LASABABISHA NDEGE YA NAHODHA KUKWAMA KUTUA

Ndege ya Serikali ikiwa imembeba Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, imeshindwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Zanzibar kutokana na giza baada ya jenereta ya kufua umeme wa dharura kuharibika.

Waziri Kiongozi alikuwa akitokea mkoani Dodoma kuhudhuria kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM akiwa amefuatana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar, Shawana Buheit Hassan ambaye pia ni mjumbe wa NEC.

Taarifa zilizopatikana zimeeleza kwamba ndege hiyo iliondoka juzi saa 12:00 jioni mjini Dodoma na ilitarajia kutua saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege Zanzibar.

Hata hivyo, kutokana na uwanja huo kuwa gizani, ndege hiyo ilizunguka mara kadhaa katika anga ya Zanzibar na baadaye kwenda kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Mamlaka ya Usalama wa Usafiri wa Anga Zanzibar, Said Sumri, alithibitisha kuwa ndege hiyo ilishindwa kutua Zanzibar ikiwa na wajumbe wa NEC.

Hata hivyo, Sumari hakutaka kuingia kwa undani zaidi juu ya suala hilo kwa madai kwamba si msemaji.

Lakini vyanzo vya habari katika tukio hilo vilieleza kwamba ndege hiyo ililazimika kuzunguka katika anga ya Zanzibar na baadaye kurejea Dar es Salaam na kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

“Tulilazimika kulala Dar es Salaam baada ya ndege yetu kushindwa kutua kutokana na tatizo la giza kufuatia jenereta ya uwanja kuharibika,” chanzo kimoja cha habari kilikaririwa kikisema.

Hata hivyo, abiria wote waliokuwemo katika ndege hiyo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, walilazimika kujihudumia gharama za hoteli na kulazimika kusafiri Zanzibar siku iliyofuata na kuwasili Zanzibar saa 4:00 asubuhi jana.

Baadhi ya viongozi waliokuwemo ndani ya ndege hiyo ni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadh Salmin (Magomeni), Ali Suleiman Ali (Kwahani), Thuwaiba Kisasi (Viti Maalum), Zainab Shomari (NEC), Issa Ahmed Othman (NEC) na wasaidizi kadhaa wa Waziri Kiongozi.

Lakini Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege Zanzibar, Malik Mohammed Hanif, alisema ndege hiyo ilishindwa kutua Zanzibar kwa vile uwanja wa ndege upo katika matengenezo.

Alisema tangu kuanza matengenezo katika uwanja huo, umekuwa ukifungwa kuanzia saa 1:00 usiku ili kuweka mazingira ya utulivu wakati mafundi wakitekeleza majukumu yao.

“Ndege ilishindwa kutua kutokana na matengenezo yanayoendelea katika uwanja huo na sio kweli kama jenereta liliharibika ghafla," alisema Mkurugenzi huyo.

Zanzibar haina huduma za umeme tangu Desemba 10, mwaka jana na kuathiri sekta za kiuchumi na kijamii, baada ya waya unaopokea umeme kutoka Tanzania Bara kulipuka katika kituo cha Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kutokana na tatizo hilo, taasisi mbalimbali zimekuwa zikitumia umeme wa dharura wa majenereta, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ambao hivi sasa upo katika matengenezo makubwa yanayofanywa na Kampuni ya Sogea Satom ya nchini Ufaransa.

Uwanja huo wa ndege unatarajiwa kuongezwa urefu kutoka mita 2,662 hadi 3,022 na mradi huo unatarajiwa kukamilika Agosti, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment