Monday, February 22, 2010

MARUBANI WA LUTHANSA WAGOMA

Shirika la ndege la kitaifa la Ujerumani, Lufthansa, limelazimika kusitisha safari zake baada ya marubani wake wote 4,000 kuanza mgomo wa siku nne kuhusu mishahara na usalama wa kazi zao.

Shirika hilo limesimamisha zaidi ya safari 3,000 za ndege zao. Msemaji wa shirika hilo Klaus Walther amesema mgomo huo utailetea kampuni hasara ya zaidi ya dola milioni 136.

Mgomo huo sasa unamanisha kutakuwa na msongamano wa abiria huku safari nyingi za ndege Barani Ulaya, zikicheleweshwa.

Chama cha marubani hao, Cockpit, kimesema kinataka wanachama wake kupewa nyongenza ya mshahara ya asilimia 6.3.

Pia kinataka Lufthansa kuwahakikishia marubani wake kuwa hawatapoteza kazi wakati ambapo kampuni hiyo itaanza kutumia makampuni mengine ya ndege kutoa baadhi ya huduma zake.

Vilevile chama hicho kinataka kupewa nafasi ya kuchangia zaidi katika maamuzi yanayofanywa na kampuni hiyo. Hadi sasa pande hizo mbili hazijaafikiana kufanya mazungumzo, lakini Klaus Walther anasema Lufthansa iko tayari kufanya hivyo.

Lufthansa inatarajiwa kufutilia mbali safari 800 za ndege kila siku, au theluthi mbili za ratiba yake. Waziri wa Usafiri wa Ujerumani Peter Ramsauer ameonya kuwa mgomo huo utaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Ujerumani na amejitolea kuwa mpatanishi wa mzozo huo wa malipo.

No comments:

Post a Comment