Saturday, February 6, 2010

BAN AZUNGUMZIA VITA VYA GAZA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema bado hakuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha iwapo Israel na Palestina zimetekeleza matakwa ya umoja huo kufanya uchunguzi wa vita vya Gaza mwaka uliopita. Taarifa iliyotolewa na Bwana Ban kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, imeeleza kuwa hakuna uamuzi unaoweza kutolewa juu ya utekelezaji wa azimio la pande zote zinazohusika.

Jana Ijumaa Israel ilisema kuwa uchunguzi wa kijeshi ilioufanya kuhusu vita hivyo ulikuwa wa kuaminika, lakini kundi la kutetea haki za binaadamu la Gaza limedai kuwa uchunguzi wa Israel haukukidhi matakwa ya Umoja wa Mataifa ya kufanya uchunguzi huru.

Taarifa zinazokinzana zimetolewa baada ya tarehe ya mwisho ya miezi mitatu iliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Israel na kundi la Hamas kuchunguza madai kwamba wanahusika katika uhalifu wa kivita wakati wa vita vya Gaza Disemba mwaka 2008 hadi Januari mwaka uliopita, kumalizika siku ya Ijumaa.

No comments:

Post a Comment