Saturday, January 30, 2010

MELI ZANZIBAR ILIZAMA KWA UZEMBE

Hatimae ripoti ya kuzama kwa meli ya LCT Fatih, iliyosababisha vifo vya watu sita katika Bandari ya Malindi imetangazwa na serikali na kuelezwa ajali hiyo imetokana na uzembe wa nahodha wake Ussi.

Akisoma ripoti ya uchunguzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mawasilano na Uchukuzi, Machano Othman Said, alisema meli hiyo ilikuwa inaingiza maji kupitia mlango wa mbele na baadaye ilizama baada ya kuelemewa na kiwango kikubwa cha maji na tani 55 za mizigo zilizokuwamo ndani ya meli.

Akiwasilisha ripoti hiyo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi alisema sehemu ya chini ya meli hiyo pia iligundulika ilikuwa na matobo yaliyokuwa yakiingiza maji na kuwa chimbuko la kuzama kwa meli hiyo.

“Mheshimiwa Spika, meli ilikuwa haina mfumo wa kuingiza maji katika matangi yake kutokana na mabadiliko ya muundo yaliyofanywa huko nyuma nchini Madagascar,” alisema.

Waziri Machano alisema wakati meli ikiwa katika hatari ya kuzama Nahodha wa meli hiyo kapteni Ussi hakuchukua hatua yoyote ya kuomba msaaada kupitia mamlaka za uokozi.

“Nahodha achukuliwe hatua za kisheria ikiwamo kushitakiwa kwa kusababisha ajali na kupoteza maisha ya watu na mali zao,” alisema Waziri Machano.

Waziri Machano alisema kwamba ukaguzi wa meli hiyo pia unaonyesha kuwepo udanganyifu mkubwa kwa kampuni iliyopewa kazi ya kuikagua meli hiyo na itachukuliwa hatua ya kutozwa faini kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aidha, meli hiyo imegundulika ilikuwa ikifanya kazi huku ikiwa ina vyeti batili, vilivyotolewa na watendaji wa Ofisi ya Mrajisi wa Meli Zanzibar.

Bodi hiyo ya uchunguzi iliongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Omar Makungu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa. Wajumbe ni Kapteni Alhaji Sururu, Mwandisi Abdi Omar Maalim, Abdallah Kombo, Kapteni Mohammed Juma na Kapteni Wilium Mlesa.

No comments:

Post a Comment