Monday, December 14, 2009

Kanisa Katoliki nchini limeanzisha utaratibu wa kusomesha mapadri wake kwenye Vyuo vikuu vya Kiislamu nchini Misri, lengo likiwa ni kujifunza Quran Tukufu na lugha ya Kiarabu.

Utaratibu huo ulioanza miaka zaidi ya mitano iliyopita una lengo la kujenga mahusiano mema na kuondoa migogoro na migongano baina ya Waislamu na Wakristo nchini, ikiwa ni njia ya kuimarisha imani ya waumini wa kanisa Katoliki

Hayo yamebainishwa na Mhashamu Baba Askofu Anthoni Banzi wa Jimbo Katoliki la Tanga, alipokuwa akimkaribisha mmoja wa mapadri waliohitimu masomo ya Quran tukufu na lugha ya Kiarabu kutoka chuo kikuu nchini Misri, Padri Benedict Shemfumbwa katika sherehe za Masista wa Bibi yetu wa Usambara zilizofanyika mwishoni mwa wiki katika makao makuu ya shirika hilo Kwamdolwa Korogwe, Tanga

Katika sherehe hizo masista saba waliweka nadhiri za daima na masista saba walisherehekea Jubilei ya miaka 25 ya kumtumikia Mungu wakati masista watatu walisherehekea Jubilei ya miaka 50 ya kumtumikia Mungu wakijifungamanisha kwa Nadhiri yao ya ufukara, na uaminifu, unyeyekevu kwa Yesu Kristo katika kulihudumia kanisa na jamii.

Akizungunza katika ibada hiyo iliyoshirikisha masista zaidi ya 300 na mapadri zaidi ya 15 wa mashirika mbalimbali ya kitawa, Askofu Banzi alisema kuwa Padri Shumfumbwa ni mtaalamu wa Quran tukufu na lugha ya Kiarabu kutoka nchini Misri na kuwa kanisa na Jimbo la Tanga linajivunia mtaalamu huyo.

‘Naomba nimtambulishe kwenu mtaalamu wa Quran Tukufu na lugha ya Kiarabu, Padri Benedict Shemfubwa amesomea nchini Misri miaka miwili halafu akaenda Roma, Italia miaka miwili…nitampatia nafasi katika Injili ya leo awapatie mahubiri lakini sio awafundishe Quran leo hapa,’’ alisema Askofu Banzi na kushangiliwa.

Askofu Banzi alisema kuwa kwa sasa Padri Shemfubwa yuko katika makao makuu ya kanisa hilo Chumbageni jijini Tanga akiishi karibu na ofisi za Jimbo Katoliki kwa lengo la Kutoa ushauri na kutekeleza elimu yake kwa vitendo pale atakapohitajika kufanya hivyo.

Akizungumza kuhusiana na watawa hao, Askofu Banzi alisema kuwa amefurahishwa na hatua ya watawa watatu ambao walisherehekea miaka 50 ya utawa wao wakiwa bado wana nguvu na wala hawatembei na mikongojo.

Baadhi ya mapadri na masista walioongea na Nipashe kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini wamesema kuwa mpango huo wa kuwa na wataalamu wa Quran Tukufu na lugha ya Kiarabu umewashirikisha pia watawa wa kike ambao pia wako nchini Misri kujifunza.

Akizungunza na Nipashe baada ya sherehe hizo Padri Shemfubwa alisema kuwa elimu yake ya Quran Tukufu na lugha ya Kiarabu aliyojifunza nchini Misri ataitumia kuleta chachu ya maridhiano baina ya waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini ili kujenga taifa moja na imara kwa kuheshimiana na kudumisha upendo.

No comments:

Post a Comment