Sunday, October 11, 2009

Idadi ya waislamu duniani inakadiriwa kufikia watu bilioni 1.57 na hivyo kumaanisha kwamba katika kila watu wanne duniani mtu mmoja kati yao ni muumini wa dini ya kiislamu.

Utafiti huu ulifanywa na taasisi ya Marekani ya Pew Forum kuhusiana na dini na maisha ya jamii katika kipindi cha miaka mitatu katika nchi 232 duniani. Baadhi ya matokeo ya utafiti huu yanaweza yakawashangaza watu wengi kutokana na ukweli uliojitokeza.


Kwa mfano Ujerumani ina waislamu wengi kuliko nchi ya kiislamu ya Lebanon, China ina waislamu wengi kuliko nchi ya kiarabu ya Syria, Urusi ina waislamu wengi kuliko nchi za Jordan na Libya zikiunganishwa pamoja wakati Ethiopia ina idadi ya waislamu sawa na Afghanistan.


"Yale mawazo kwamba waislamu ni waarabu na waarabu ndio waislamu yameonyesha kutokuwa na ukweli wowote kwa kuzingatia ripoti hii", alisema Amaney Jamal, profesa msaidizi wa masuala ya siasa katika chuo kikuu cha Princeton University ambaye alipewa nakala ya mwanzo ya matokeo ya utafiti huo.


Matokeo ya utafiti huu yalipatikana kwa kuzingatia ripoti za sensa za nchi husika na utafiti uliofanyika katika nchi hizo 232. Utafiti huo pia ulionyesha kwamba waislamu wa madhehebu ya Shia ni kati ya asilimia 10 na 13 ya waislamu wote duniani. Asilimia 80 ya waislamu wa dhehebu la shia wanaishi Iran, Pakistan, India na Iraq.


Taarifa ya ripoti hiyo ilionyesha pia kwamba ingawa moyo wa uislamu unaweza ukawa mashariki ya kati kwenye nchi za kiarabu lakini idadi kubwa ya waislamu zaidi ya asilimia 60 wanaishi bara la Asia.Asilimia 20 ya waislamu wanaishi katika nchi za mashariki ya kati na nchi za kaskazini mwa Afrika.


Asilimia 15 wanaishi nchi za ukanda wa jangwa la sahara, asilimia 2.4 wanaishi barani ulaya na asilimia 0.3 wanaishi kwenye bara la Amerika. Nchi yenye waislamu wengi kuliko nchi zote duniani ni Indonesia yenye waislamu milioni 203 ambayo ni asilimia 13 ya waislamu wote duniani.


India ambayo inashika nafasi ya tatu kwa idadi kubwa ya waislamu duniani ina waislamu milioni 161 lakini idadi hiyo ya waislamu ni asilimia 13 tu ya raia wote wa India.Katika utafiti huo Tanzania imo kwenye orodha ya nchi zenye waislamu wengi na imetajwa kuwa na waislamu wapatao milioni 13.


Ingawa idadi ya wakristo duniani inasemekana kuwa kubwa kuliko ya waislamu, utafiti kama huu utafanyika kuanzia mwakani kugundua idadi ya kweli ya wakristo duniani.

No comments:

Post a Comment