Sunday, July 25, 2010

Asilimia 23 ya watu wazima Lesotho na Msumbiji ni waathirika wa maradhi ya Ukimwi.

Mkutano wa 18 wa kimataifa wa ukimwi unafungwa rasmi hii leo mjini Vienna Austria,huku suala la msongamano wa wafungwa magerezani,likitajwa kuwa chanzo kikubwa cha kusambaa kwa maradhi hayo.

Mkutano huo pia umejadili masuala kadhaa juu ya jinsi ya kukabiliana na ugonjwa huo,ambao umegeuka tishio zaidi duniani.

Tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani,limetajwa kuwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya kusambaa kwa ugonjwa huo,lakini pia Mkutano huo umeelezwa kuwa uchangiaji wa sindano na michoro ya alama za tattoo kuwa nayo yanachangia kusambaa kwa virusi hivyo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa kitengo cha ofisi ya umoja wa mataifa kinachoshughulikia madawa ya kulevya na uhalifu,wameeleza kuwa zaidi ya watu milioni 30 duniani,wameambukizwa maradhi hayo kutokana na matatizo ya msongamano wa magereza,huku matukio ya kuwepo kwa vitendo vya ngono na ulawiti vikitajwa kuchangia zaidi hali hiyo,kutokana na kukosekana kwa mipira ya kondomu.

Katherine Todrys aliyesimamia utafiti wa shirika la haki za binaadamu la Human right Watch,katika magereza 6 ya Zambia,ameeleza kuwa nchi hiyo imeshindwa kabisa kuwa na mkakati maalumu wa kuwapima wafungwa afya zao.

Mkutano huo umeelezwa kuwa hali ni mbaya zaidi nchini Zambia,ambapo watumishi 14 wa afya,wanahudumia zaidi ya wafungwa 15,300,katika magereza 86 nchini humo,na kueleza kuwa dawa pekee inayopatikana kwa wafungwa hao ni ya kutuliza maumivu na inayopunguza homa,hali inayohatarisha afya za wafungwa,hasa walioathirika na virusi vya Ukimwi.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na serikali ya Marekani mwaka 2008,imetaja kuwa zaidi ya asili mia 27 ya wafungwa nchini Zambia ni waathirika wa Ukimwi,ikiwa ni mara mbili ya wale walio nje ya magereza.

Kwa upande wa Nigeria,wanaharakati kutoka asasi ya uzazi wa mpango,wameeleza kuwa wanakabiliwa na hali ngumu katika kusambaza mipira ya kondomu,kutokana na imani za walio wengi,kuamini kuwa kitendo hicho ni sawa na kuchochea vitendo vya ngono.

Wakati huo huo,imeelezwa kuwa kutoa matibabu kwa kutumia timu ya wanajamii waishio vijijini kwa wagonjwa wapya wa ukimwi barani Afrika,ndio suluhisho pekee la kukabiliana na maradhi hayo,tofauti na kutegemea madaktari.

Imeelezwa kuwa timu ya wanajamii waishio vijijini,wanaweza kusaidia kupunguza gharama,na kuwasaidia waathirika wa Ukimwi,kuishi muda mrefu zaidi,kuliko wale ambao wanachelewa kupatiwa matibabu hayo,kwa kutegemea madaktari kutoka maeneo ya mbali.

Kitengo cha utafiti cha MSF;kilichofanya utafiti huo nchini Msumbiji na Lesotho kimefahamisha kuwa asilimia 23 ya watu wazima ni waathirika wa maradhi ya Ukimwi.

Daktari Helen Bygrave wa Medisins San Frontieres,MSF nchini Lesotho,amesema kuwa kati ya waathirika 1,128 wanaoishi maeneo ya vijijini nchini humo,asilimia 70 kati ya hao,wana uwezekano mkubwa wa kufariki katika kipindi cha miaka 2 ijayo,kuliko waathirika ambao waliwahi kupatiwa huduma ya matibabu kabla yao.

Ugonjwa wa ukimwi kwa mara ya kwanza uligunduliwa mwaka 1981 na kwamba kabla ya kuanza kutumika kwa dawa hizo za kupunguza makali ya ugonjwa,watu walianza kuugua ugonjwa huo ndani ya kipindi cha miaka kumi toka kupata maambukizo na hufariki baada ya mwaka mmoja au miwili.

Mkutano wa 18 wa kimataifa kuhusu ukimwi,umehudhuriwa na wataalamu wapatao 25,000, wakiwemo kutoka sekta za afya na watunga sera, ili kujadiliana hatua mbalimbali katika mapambano dhidi ya ukimwi na kuangalia njia za kuweza kutoa kinga zaidi na matibabu dhidi ya virusi vinavyosababisha ukimwi.

***DW - Deutsch Welle

No comments:

Post a Comment