MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, atajulikana Julai 9 mwaka huu mjini Dodoma, wakati Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama hicho, itakapokutana na kupiga kura kumpata mgombea huyo.
Kwa mujibu wa Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya NEC, John Chiligati, siku inayofuata mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM atapigiwa kura na Mkutano Mkuu na ndipo pia mgombea mwenza atajulikana.
Chiligati alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa taarifa ya kikao cha siku moja cha kawaida cha NEC kilichokutana juzi kujadili masuala mbalimbali ukiwamo Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika Julai 10 na 11, mwaka huu.
“Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa CCM utakaofanyika Julai 10 na 11 yanakwenda vizuri … mkutano huo ndio utakaopiga kura ya kuchagua mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kama watajitokeza wagombea wengi, zitapigwa kura na kama atajitokeza mmoja, pia zitapigwa kura za Ndiyo na Hapana, ili litoke jina la mgombea urais,” alisema Chiligati na kuongeza:
“Halmashauri Kuu ya Taifa itakaa Julai tisa kuchagua mgombea urais wa Zanzibar na tutakwenda katika Mkutano Mkuu kuchagua mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hapa tutajua mgombea mwenza na CCM itakuwa na timu kamili.”
Hadi sasa, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyejitokeza kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, akielekea kuwa mgombea pekee wa kiti hicho kwa chama hicho ambacho kimepanga Julai mosi kuwa siku ya mwisho ya kuchukua na kurudisha fomu za kuwania kiti hicho.
Akizungumzia masuala mengine yaliyojadiliwa na NEC, Chiligati alisema walipokea malalamiko 163 kuhusu rafu zinazodaiwa kuchezwa katika majimbo mbalimbali wana-CCM waliotangaza nia pamoja na wabunge wa sasa.
Alisema malalamiko hayo yanashughulikiwa kwa ngazi mbalimbali yakiwamo 40 yaliyopelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa sababu yanahusu rushwa.
Aidha, Chiligati alisema kura za maoni kwa wanachama wa CCM wanaotaka kuwania ubunge katika majimbo zitafanyika Agosti mosi mwaka huu; takriban wiki mbili baada ya Bunge la Tisa kuvunjwa Julai 16, kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.
Alisema CCM imesogeza mbele uandikishaji wa wanachama na upokeaji wa wanachama wapya katika Daftari la Wanachama litakalotumika katika kupiga kura za maoni kuanzia Juni 30 hadi Julai 15 mwaka huu, baada ya watu wengi kujitokeza.
Mbali na hayo, CCM pia imebadilisha utaratibu wa mgawo wa viti maalumu vya ubunge katika mikoa ambapo sasa mikoa itakuwa na viti viwili kama ilivyo sasa, badala ya vitatu vilivyopangwa awali, kutokana na kuongezwa kwa mikoa mipya mitatu ya Simiyu, Geita na Njoluma.
Naye Amir Mhando anaripoti kutoka Zanzibar kwamba
mfanyabiashara maarufu mjini hapa, Mohammed Raza amechukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar kupitia CCM na kusema atahakikisha kila jimbo linapata zahanati kwa ajili ya wajawazito.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana, Raza aliyepata kuwa Mshauri wa Michezo wa Rais wa Awamu ya Tano wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, alisema ataleta maendeleo na atasimamia pia umoja, mshikamano na kuwaunganisha Wazanzibari.
"Nikishapata nafasi ya kuwa Rais, nitaacha biashara zangu zote, maana siasa na biashara haziendani, pia katika Serikali yangu nitaweka wasaidizi waadilifu, nitasimamia utawala bora, nitahakikisha haki za binadamu zinafuatwa na maadili ya kazi yanakuwapo.
"Kutokana na ukereketwa wangu wa CCM nimezunguka majimbo yote 50 ya Unguja na Pemba, jambo nitakalolipa kipaumbele ni huduma za afya, nitaweka zahanati katika kila jimbo la Zanzibar.
"Pia kila jimbo nitaweka kituo cha kompyuta kwa ajili ya masuala ya kijamii, nitapanua wigo wa kutafutia soko wafanyabiashara wadogo, nasema maisha bora kwa kila Mzanzibari yanawezekana,
nitaweka sera maalumu kwa wafanyabiashara hao wapate mikopo," alisema Raza.
Aliwaomba wananchi wa Zanzibar kuhakikisha wanaheshimiana kwani malumbano hayawasaidii na kuongeza kuwa kwa imani yake hakuna mwana halali wa Zanzibar asiyetaka amani na mshikamano.
Alisema akipitishwa na CCM, akachaguliwa urais wa Zanzibar atashirikiana na viongozi wenzake kutatua kero za Muungano, alizoeleza kuwa zitamalizika kwa mazungumzo.
Alipoulizwa kwamba haoni kama CCM inaweza isimpitishe kwani ni miongoni mwa wagombea wasiopewa nafasi alijibu: "CCM ni chama makini, hakuna matabaka, wewe ukisema mimi ni Mhindi au Mwarabu sipitishwi si sahihi, sote ni Wazanzibari, tuache masuala ya matabaka."
Wanachama wanane wa CCM walikuwa wamechukua fomu kabla ya jana ili kuwania urais wa Zanzibar kupitia CCM; Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Ali Abeid Karume, Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna.
Wengine ni Kamishina mstaafu wa Utamaduni, ambaye amepata kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Hamadi Bakari Mshindo, Waziri Kiongozi mstaafu Dk. Mohammed Gharib Billal na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud na Mbunge wa Chumbuni, Omari Sheha Mussa.
Wanachama wengine wawili licha ya Raza walitarajiwa kuchukua fomu jana ni Waziri wa Elimu Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman na Mohammed Yusuph, ambaye haikuelezwa wadhifa wake.
Kulingana na taratibu zilizowekwa na CCM, wanachama hao wanatakiwa kutafuta wadhamini 250 katika angalau mikoa mitatu ya Zanzibar na kati ya hiyo, mmoja lazima uwe wa Pemba na mwisho wa kurudisha fomu ni Julai mosi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment