Wednesday, May 26, 2010

TAIFA STARS VS RASIL JUNI 2 DAR

Timu ya soka ya Taifa ya Brazil inatarajiwa kutua nchini kwa ajili kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakayopigwa Juni 2 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, alisema mazungumzo ya ujio huo yanaendelea chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.

Tenga alisema, timu hiyo itakayokuwa njiani kuelekea Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia, itasaidia kupitia mechi hiyo kukinoa kikosi cha Stars kitakachokuwa kikijiandaa na mechi yake ya marudiano na Rwanda ‘Amavubi’.

“Ujio wa Brazil utakuwa na manufaa kwetu, kwani utasaidia kuipa mazoezi timu yetu ya taifa ambayo baada ya hapo itaelekea Rwanda kucheza mechi yao ya marudiano,” alisema.

Katika hatua nyingine, Tenga aliipongeza timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ kwa kushinda mechi yao ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake, baada ya kuitandika Eritrea kwa mabao 8-1 mwishoni mwa wiki.

Tenga alisema, ushindi huo usiwafanye wabweteke, kwani wapinzani wao watakwenda kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya mechi yao ya marudiano, hivyo kufanya mchezo kuwa mgumu zaidi.

Wakati huohuo, tiketi 380 za mashabiki waliojiandikisha kwenda Afrika Kusini kushuhudia fainali za Kombe la Dunia, zimeishawasili jijini ambapo TFF inawahimiza wahusika kwenda kuzichukua.

.

1 comment:

  1. Kila Timu ikija kucheza mechi za kirafiki inakosa kuwa mabingwa mfano ni IVERY COAST imeukosa ubingwa wa Africa na Timu yao ni nzuri, sasa hao Brasil pia wataukosa ubingwa wa Dunia. i unajua jina letu almaarufu "KICHWA CHA MWENDAWAZIMU" kwa hiyo tunapocheza na wenzetu mechi ya kirafiki tunawaambukiza huu ugonjwa wetu.mdau Leicester uk shemejiii!!!. inishiii!!

    ReplyDelete