Friday, April 16, 2010

SAFARI KADHAA ZA NDEGE BARANI ULAYA ZAAKHIRISHWA

Wingu kubwa la majivu yanayotoka katika mripuko wa Volcano huko Iceland, limesababisha kuahirishwa kwa safari za ndege zipatazo elfu saba barani Ulaya.

Maelfu ya wasafiri wamekwama katika viwanja vya ndege, wakati mamlaka zikilazimika kuzizuia ndege hizo kuruka.

Msemaji wa shirika linaloratibu safari za ndege barani Ulaya -Eurocontrol- amefahamisha kuwa tatizo hilo linaweza kuendelea hadi leo.

Wakati wingu hilo la majivu likielekea kusini mashariki mwa Ulaya, kutokea Iceland, anga za nchi za Scandnavia, Uingereza, Holand na Ubelgiji, zimefungwa, isipokuwa kwa ndege za dharura tu.

Wingu hilo pia limezifikia Ujerumani, Ufaransa na Poland ambapo viwanja vya ndege vilivyoathiriwa vimefungwa.

Nako nchini Ujerumani viwanja vya ndege katika miji ya Hamburg, Hanover na Bremen vitaendelea kufungwa mpaka saa mbili asubuhi hii leo, kwa saa za Ujerumani.

Uwanja wa ndege wa Düsseldorf pia umeathiriwa na hali hiyo, huku ndege kadhaa zikiahirisha safari katika uwanja wa ndege wa Frankfurt, ambao ni wa tatu kwa shughuli nyingi barani Ulaya.

Nako nchini Holland uwanja wa ndege wa Schipol umefungwa pia kufuatia mataizo hayo ya hali ya hewa, huku abiria kadhaa wakionekana kutafuta hoteli za kulala mpaka hapo viwanja vitakapofunguliwa tena.

Mamlaka husika zimekuwa zikichunguza hali hiyo.

.

No comments:

Post a Comment