Thursday, March 4, 2010

UMOJA WA MATAIFA KUONDOA ASKARI WAKE CONGO


Umoja wa Mataifa umesema umeanzisha majadiliano na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu kuondolewa kwa awamu kwa vikosi vya kulinda amani.

Operesheni ya Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUC, ndiyo yenye idadi kubwa ya wanajeshi wanaolinda amani katika operesheni zote za kulinda amani duniani za Umoja wa Mataifa.

Muda wa vikosi hivyo unatarajiwa kumalizika mwezi May.

Tangazo hilo lilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anayeshughulikia operesheni za kulinda amani, Alain Le Roy, baada ya mkutano na Rais Joseph Kabila.

Hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu tarehe ambapo wanajeshi hao wataanza kuondolewa, lakini serikali ya Congo inataka waondolewe mwaka huu.

Bw Le Roy alisema kundi la Umoja wa Mataifa lilipatiwa muda wa mwezi mmoja kutathmini jinsi walinda amani hao wanaweza kuanza kuondoka Congo, kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kuongezewa muda kwa MONUC, mwezi June.

Msemaji wa serikali ya Congo, Lambert Mende, amesema askari wa kulinda usalama wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kuondoka nchini humo isipokuwa mkoa wa mashariki wa Kivu ifikapo mwisho wa mwaka huu.



No comments:

Post a Comment