Wednesday, March 24, 2010

NETANYAHU AKUTANA NA OBAMA

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasili katika Ikulu ya Marekani ya Whitehouse atakakokutatana na Rais Barack Obama.

Rais Obama na bwana Netanyahu wanakutana kwa mara ya kwanza tangu serikali za Marekani na ile ya Israeli kutofautiana hadharani hivi karibuni, kuhusu mpango wa Israeli wa ujenzi wa makazi mapya ya wayahudi mashariki mwa Jerusalem.

Mkutano huo unafanyika baada ya Waziri Mkuu Netanyahu kulihutubia bunge la
Marekani alikosisitiza kuwa mchakato mzima wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati ya kudumu huenda ukakwama kwa mwaka mmoja mwengine ikiwa Wapalestina hawatolitupilia mbali dai lao la kusimamishwa kabisa ujenzi wa makazi ya walowezi.

Wakati wa ziara yake nchini Marekani Bwana Netanyahu amerejelea kile alichosema ni haki ya Israeli ya kujenga mjini Jerusalem.

''Jerusalem ni mji mkuu wa Israeli na si makazi'', alieleza Bwana Netanyahu.


Awali, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo wa nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa jumla zinaamini kuwa sera ya Israel ya kuendelea kuyaongeza makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo la Jerusalem Mashariki inazirudisha nyuma hatua zozote zile za kufikia amani ya Mashariki ya Kati.

.

No comments:

Post a Comment