Tuesday, March 30, 2010

MAMA SALMA KIKWETE ANUSURIKA AJALINI

Mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete, amenusurika kupata ajali baada ya msafara wake kugongwa na lori linalodaiwa kuwa lilikuwa limebeba bidhaa za magendo.

Lori hilo linadaiwa kuuvamia msafara huo na kusababisha baadhi ya magari yaliyokuwapo kugongana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Tanzania Daima, hakuna mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo zaidi ya magari yaliyokuwa katika msafara huo kuharibika.

Taarifa hizo zilibainisha kuwa ajali hiyo ilitokea jana asubuhi muda mfupi wakati msafara huo ukitokea Wilaya ya Tarime, mkoani Mara ukielekea Rorya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ajali hiyo ilitokea baada ya lori ambalo namba zake za usajili hazijafahamika mara moja likiendeshwa kwa mwendo wa kasi, kukaidi amri ya askari wa kikosi cha usalama barabarani kulitaka lisimame kwa ajili ya kupisha msafara wa mke wa rais.

“Lori ambalo namba zake hazijafahakamika mara moja liliingia kwenye msafara wa Mama Salma Kikwete, kutokana na kukaidi amri ya askari wa usalama barabarani kumtaka dereva kuupisha msafara huo,” kilisema chanzo cha habari.

Kiliongeza kwamba, baada ya kukaidi amri ya askari wa kikosi cha usalama barabarani, likiwa kwenye mwendo wa kasi liliingilia masafara wa Mama Salma Kikwete na kuligonga gari mojawapo na kwenda pembeni mwa barabara.

Imedaiwa kugongwa kwa gari hiyo ya tatu kutoka kwa mke wa kiongozi wa nchi, ilisababisha magari mengine yaliyokuwa nyuma ya msafara huo kugongana yenyewe kwa yenyewe.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, waliiambia Tanzania Daima kwamba, lori hilo lilishindwa kusimama kama lilivyoamriwa kutokana na kubeba bidhaa za magendo.

Mashuhuda hao waliongeza kwamba dereva wa lori hilo alikuwa akikimbia askari wa usalama kwa kuhofia kukamatwa akiwa na bidhaa za magendo.

“Lori lilishindwa kusimama kama lilivyoamriwa kutokana na kubeba bidhaa za magendo, dereva wa lori hilo alikuwa akikimbia askari wa usalama kwa kuhofia kukamatwa akiwa na bidhaa za magendo,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Tanzania Daima ilijaribu kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime, Costatine Massawe kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kupokewa na msaidizi wake na kudai yuko kwenye mkutano.

“Kamanda yupo kwenye kikao labda mpigie kuanzia saa moja usiku, mimi siwezi kuzungumza juu ya ajali unayoiulizia,” alisema msaidizi huyo.

Aidha Msemaji wa Jeshi Polisi nchini, Abdallah Msika aliithibitishia Tanzania Daima kutokea kwa ajili hiyo, lakini alishindwa kutoa maelezo zaidi kwa madai hajapata taarifa za kina.

Kamanda Msika alisema alikuwa nje ya ofisi na aliporudi alijaribu kuwasiliana na makamanda wa mikoa ya kipolisi ya Tarime na Rorya bila mafanikio kutokana na kuwepo kwenye mikutano.

Alibainisha kuwa baada ya kushindwa kuwapata makamanda hao, aliwasiliana na maofisa kadhaa ambao walimthibitishia kutokea kwa ajali hiyo.

“Ni kweli ndugu yangu mke wa mheshimiwa rais amepata ajali, lakini hakuna aliyefariki na pia sikuweza kupata taarifa za kina zaidi,” alisema Msika.

Aliliahidi Tanzania Daima kuwa, atafuatilia kwa karibu suala hilo, lakini mpaka tunakwenda mitamboni alishindwa kufanya hivyo kutokana na kutopatiwa taarifa na wahusika waliokuwapo eneo la tukio.

***Tz Daima

No comments:

Post a Comment