Thursday, March 18, 2010

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBA KUHUSU UMEME



SHUKURANI ZA RAIS WA ZANZIBAR NA

MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,

MHESHIMIWA DK. AMANI ABEID KARUME,

KWA WANANCHI KUHUSU KUREJEA KWA

HUDUMA YA UMEME, UNGUJA,

TAREHE 18 MACHI, 2010



Ndugu Wananchi,

Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Muweza wa kila kitu na Mwenye Wingi wa Rehma, kwa kutuweka salama na katika hali ya amani na utulivu kwa kipindi chote ambacho kisiwa chetu cha Unguja kilikosa huduma ya umeme. Pia, namshukuru kwa kutuwezesha kufanikisha juhudi za kuirejesha huduma hiyo. Ni wajibu wetu kumshukuru kwa hayo.

Ndugu Wananchi,

Ni vyema nikaelezea hali halisi iliyosababisha kukosekana huduma ya umeme katika kisiwa cha Unguja kwa muda huo wa miezi mitatu.

Kama mnavyofahamu, Kisiwa chetu kinapata huduma ya umeme kwa kutumia waya uliopitishwa chini ya bahari na kuunganishwa na Gridi ya Taifa kutoka Tanzania Bara. Waya huo ulioanzia Rasi Kiromoni (Tanzania Bara) hadi Fumba (Unguja) wenye urefu wa kilomita 37.5 na uwezo wa kuchukua umeme wa nguvu ya Megawati 45, ulijengwa chini ya mradi mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mwaka 1979 ili kuondoa kabisa matatizo ya umeme ya wakati huo na kwa miaka mingi iliyofuatia.

Tarehe 21 Mei, 2008 kwa mara ya kwanza huduma ya umeme kisiwani Unguja ilikatika ghafla kutokana na kuharibika kwa sehemu ya waya huo.

Serikali yenu ilichukua juhudi kubwa na za haraka kuirejesha huduma hiyo, na baada ya matengenezo makubwa yaliyofanywa na wataalamu kutoka Norway na Afrika Kusini, tarehe 18 Juni, 2008 umeme ulirejea kama kawaida. Baada ya tatizo hilo, Serikali iliongeza nguvu zake za kuandaa mikakati bora ya kuimarisha vituo vya Rasi Kiromoni na Fumba kwa matengenezo ya miundo mbinu na ililazimika kuingia mkataba na kampuni ya EHT Cables ya Afrika Kusini ili kuongeza nguvu za kitaalamu katika matengenezo ya kawaida na ya dharura ya mitambo hiyo.

Mnamo tarehe 3 Disemba, 2009 kulibainika kuvuja kwa mafuta katika kiungo kilichofanyiwa matengenezo hapo awali. Wataalamu wa Shirika letu la Umeme wakishirikiana na wataalamu kutoka Afrika Kusini waliweza kutengeneza kiungo hicho tarehe 12 Disemba, 2009. Huduma ya umeme ilirejea tena ingawa muda mfupi baadae matatizo ya kukatika kwa waya mwengine yalijitokeza na kusababisha mripuko na maharibiko makubwa zaidi.

Ndugu Wananchi,

Baada ya kutokea hitilafu hiyo, tuliwasiliana na kampuni ya Nexans ya Norway iliyotengeneza waya huo zaidi ya miaka 30 iliyopita na kuwataka ushauri wao juu ya hatua ya kuchukua ili tufanikiwe. Baada ya kufanya utafiti wa kutosha, Nexans ilituarifu kwamba maharibiko yaliyotokea yalisababishwa zaidi na uchakavu wa miundo mbinu iliyopo ya uletaji na upokeaji wa umeme kutokana na umri wake.

Baada ya mashauriano ya kitaalamu baina ya wataalamu wa ndani na nje, pendekezo la kubadilisha mfumo wa uletaji na upokeaji umeme Ras Kiromoni na kituo cha Fumba, ikiwa ndio njia pekee ya kuokoa waya ule lilitolewa na kukubaliwa na Serikali.

Hatua za utekelezaji zikiwemo uagiziaji na usafirishaji wa vifaa kutoka Sweden, Uingereza na Afrika Kusini, zilifanywa kwa ushirikiano mkubwa na mabingwa hao. (Kampuni ya Nexans ya Norway, Elmeridge Cable Service Ltd. ya UK, Erricson Network Technologies AB ya Sweden, EHT Cables ya Afrika Kusini na ZECO Zanzibar). Mpaka kufikia mwezi wa Februari 2010, jumla ya T.Shs. 755.65 milioni zimetumika kwa ununuzi wa vifaa, usafirishaji wake pamoja na malipo ya mafundi kutoka nje ya nchi. Gharama zote zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Inasikiwa kuwa gharama hizi zitazidi kutokana na matengenezo ya ziada ya miundo mbinu ya waya za juu yaliyosababishwa na hujuma na wizi uliofanywa na wahalifu na waharibifu. Hali ambayo kwa kiasi fulani imechelewesha kurejea kwa huduma ya umeme katika baadhi ya sehemu.

Ndugu Wananchi,

Wakati hatua za kurejesha umeme zikiendelea, serikali yenu ilichukua juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa huduma muhimu kama maji, afya, habari na ulinzi zinatolewa wakati wote kama tulivyofanya mwaka 2008.

Kwa upande wa huduma ya maji, afya na habari, jumla ya jenereta 44 za dharura ziliwekwa katika vituo husika. Gharama za uendeshaji wa vituo hivyo kwa miezi mitatu ni T.Shs. 1,010.2 milioni ambazo zote zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi.

Ndugu Wananchi,

Wakati serikali yenu inahangaikia utatuzi wa janga la ukosefu wa umeme nchini, maneno mengi yamesemwa, na baadhi ya watu wasiotutakia mema walidiriki kusema na kuandika kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikutoa taarifa sahihi juu ya maharibiko yaliyotokea na kwamba utengenezaji wake utachukua zaidi ya miezi sita, kwa hivyo tusahau kabisa kupata huduma ya umeme ndani ya kipindi kilichoahidiwa. Pamoja na matamshi kama hayo ya kuwavunja moyo wananchi wa Zanzibar kwa makusudi, nafuraha kusema kuwa hamkuvunjika moyo na mliendelea kuvumulia huku mkiamini maelezo sahihi yaliyotolewa na serikali yenu.

Napenda kuwapongeza sana kwa moyo wenu wa kizalendo na wakati huo huo nakushukuruni nyote kwa uvumilivu wenu, na kwa bahati nzuri sote tumeshuhudia ilipofika tarehe 8 Machi huduma ya umeme imerudi. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tuwapongeze mafundi wote wa nje na ndani walioshirikiana pamoja na kufanikisha mradi huo.

Ndugu Wananchi,

Sasa nataka niwape taarifa ya hatua za ziada tulizochukua kuhakikisha kuwa visiwa vyetu vya Zanzibar, Unguja na Pemba vitaendelea kupata umeme wa uhakika kwa miaka mingi ijayo.

Hatua ya kwanza: Baada ya kutokea matatizo ya kukatika umeme mwaka 2008, serikali yenu iliamua kuanzisha kituo cha kuzalisha umeme wa dharura wa Megawati 45 Mtoni. Kwa kushirikiana na Washirika wetu wa Maendeleo kutoka Norway, Sweden na Uingereza, kwa pamoja wamechangia jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 11.50 (Norway 4.00 milioni, Sweden 4.50 milioni, UK 3.00 milioni), mchango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 1.50 milioni kwa mradi huo.

Kituo cha Mtoni, kitakua na majenereta ya akiba 32 yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 25 sawa na asilimia 60 ya mahitaji yetu. Mikataba yote imeshatiwa saini na hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo zimeanza. Tegemeo letu ni kwamba ifikapo mwezi wa Juni mwaka huu mitambo hiyo itakua tayari kufanya kazi wakati wa dharura.

Pili: Pamoja na hatua hiyo muhimu ya kuwa na umeme wa hakiba, serikali yenu ilitambua kuwepo kwa kasi kubwa ya maendeleo nchini inayoambatana na mahitaji ya ziada ya umeme, na kwa makusudi mwaka 2008 tuliomba msaada wa ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme kupitia baharini hadi Zanzibar, kutoka Serikali ya Marekani kupitia shirika lake la Changamoto la Millenia (MCC).

Kwa bahati nzuri mradi huo wenye uwezo wa Megawati 100 umekubaliwa na hatua za utekelezaji zimeshaanza. Mradi huo utagharimu T.Shs. 84.06 bilioni zitatolewa na Shirika la MCC na T.Shs. 4.00 bilioni zitatolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Tegemeo letu ifikapo mwaka 2012 mradi huo utakamilika na kuanza kazi.

Kwa upande wa Pemba, hatua za kukamilisha mradi wa umeme kutoka Tanga hadi Pemba zinakaribia kumalizika na ifikapo mwisho wa mwezi wa Aprili kisiwa cha Pemba kwa mara ya kwanza katika historia kitapata umeme kutoka Tanga. Gharama za mradi huo ni Dola za Kimarekani 75.00 milioni (Serikali ya Norway Dola 60.00 milioni, Serikali ya Jamhuri ya Muungano Dola 5.00 milioni na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dola 10.00 milioni). Majenereta ya Wesha (Pemba) yatafanyiwa ukarabati mkubwa ili yatoe huduma wakati wa dharura tu.

Ndugu Wananchi,

Juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Awamu ya Sita, zitaiwezesha nchi yetu kuwa na miundo mbinu ya umeme wa uhakika zaidi, pamoja na mawasiliano ya kisasa. Kwa taarifa yenu, waya mpya za umeme wa chini ya bahari zitabeba waya wa ziada wa mawasiliano ya kisasa (optic fibre) na kuiunganisha Zanzibar (Unguja na Pemba) na mtandao wa kimataifa unaopita chini ya bahari. Kukamilika kwa miradi ya ulazaji wa nyaya mpya za umeme zenye nguvu na uwezo mkubwa zaidi kwa Unguja na Pemba, pamoja na upatikanaji wa majenereta ya akiba kutatuweka katika hali nzuri ya kuwa na umeme wa uhakika utakaokidhi mahitaji yetu kwa miaka mingi ijayo.

Hatua hiyo itatoa nafasi kwa serikali na wananchi kushughulikia uwekezaji katika miradi mbali mbali ya kiuchumi na uimarishaji wa huduma za jamii inayohitajia nishati ya umeme.



Shukrani:

Ndugu Wananchi,

Wakati tukikabiliwa na matatizo ya umeme, wamejitokeza wananchi wengi, makampuni binafsi pamoja na taasisi za kimataifa waliotusaidia kwa njia moja au nyengine katika kukabiliana na hali hiyo. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirika la Denmark DANIDA kwa mchango mkubwa waliotoa kuendesha majenereta ya hospitali zetu kubwa Mnazi mmoja, Kivunge na Makunduchi. Nalishukuru Shirika la UNICEF kwa mchango wake wa majenereta 12 kati ya 44 niliyoyaeleza hapo awali.

Kadhalika nawashukuru sana Washirika wetu wa Maendeleo wakiwemo Serikali ya Marekani, Sweden, Norway, Uingereza na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa msaada wao pamoja na mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya nishati ya umeme hapa Zanzibar.

Nawashukuru sana wafanyabiashara mbali mbali wakiwemo wenye maduka, mahoteli, viwanda na makampuni ya kutoa huduma kama zile za mawasiliano kwa ustahamilivu, juhudi na ujasiri wao wa kuendeleza shughuli zao kwa kutumia njia mbadala za kupata nishati ya umeme kama vile majenereta.

Aidha, natoa shukurani kwa wavuvi, wakulima na wafanyabiashara ndogo ndogo wakiwemo wauzaji wa nyama, samaki, matunda, mboga na vyakula vyengine, ambao kwa jumla, jitihada zao zilipelekea upatikanaji wa vyakula na bidhaa nyengine muhimu zinazohitajika katika maisha ya kila siku ya mwanadamu bila ya usumbufu mkubwa.

Natoa shukurani kwa wizara, mashirika, maidara, taasisi na watu binafsi waliosaidia upatikanaji wa huduma za maji kwa namna moja au nyengine katika kipindi hicho chote.

Ndugu Wananchi,

Kwa niaba yenu napenda kuwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara zifuatazo: Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Polisi pamoja na Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashirikiano ya karibu sana wakati wa kipindi chote cha dharura. Aidha, nawapongeza mafundi wote wa ndani na nje kwa kufanyakazi kwa bidii na kurejesha huduma ya umeme ndani ya muda walioahidi.

Mwisho, nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wote pamoja na wageni mbali mbali waliotembelea nchi yetu kwa uvumilivu wenu mkubwa na wa kupigiwa mfano katika kipindi chote cha kukosekana kwa huduma ya umeme hapa nchini kwetu.

Tumuombe Mwenyezi Mungu atuepushe na mitihani mizito kama iliyopita, kwa siku zijazo.

Mwenyezi Mungu awabariki wote.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.


.

No comments:

Post a Comment