Monday, March 22, 2010

MSWADA WA AFYA WAPITISHWA MAREKANI

Bunge la waakilishi mjini Washington, Marekani limepitisha mswada wa afya wa Rais Barack Obama ambao ulikua na mabishano makubwa nchini humo, mswada unaotazamiwa kuwa mkubwa zaidi katika mabadiliko yanayofanyiwa sheria za kijamii nchini humo.

Kulitokea shangwe upande wa Demokrats katika bunge walipopata kura zilizohitajika ili kupitisha mswada huo. Akimalizia kampeini za mjadala juu ya mswada huo, spika wa bunge Nancy Pelosi alisema kuwa bunge la Marekani linafikia hatua ya kihistoria.

Kwa ushindi mwembamba wa kura 219 kwa 212, Wabunge kupitia chama cha Democrats wamepigia kura mpango wenye lengo la kuwapatia bima ya afya asilimia 95 ya Wamarekani ambayo ni sawa na idadi ya watu milioni 32 ambao hivi sasa hawana kinga yoyote. Mradi huo utaigharimu serikali dola trilioni mbili na nusu.

Kwa sasa mpango huo unahitaji kusainiwa na Rais Barack Obama ili kuweza kuwa sheria.

Mwandishi wa BBC mjini Washington amesema kuwa nafasi za rais Barack Obama kupata ushindi ziliongezwa baada ya kuafikiana na wanademokrats waliopinga kutumiwa fedha za hazina ya umma katika uavyaji mimba.

Mjadala wa mswada huu ulipamba moto huku wanaharakati walioupinga wakifanya maandamano nje ya majengo ya bunge.


.


.

No comments:

Post a Comment