Wednesday, February 10, 2010

WAZIRI AKOSA LA KUJIBU BUNGENI

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremiah Sumari, jana alilishangaza Bunge baada ya kutoa jibu ambalo halikutarajiwa na wabunge.

Naibu waziri huyo alisema kuwa “hajui” mara baada ya kuulizwa swali na Mbunge wa Magogoni, Vuai Abdallah Khamis (CUF), aliyetaka kufahamu kwa nini kodi inayokatwa kwa wafanyakazi wa Zanzibar kwenye Serikali ya Muungano isibaki visiwani Zanzibar.

“Spika, napenda kumjibu mheshimiwa Mbunge kuwa sijui,” jibu hilo la Sumari lilisabaisha wabunge kuangua vicheko huku mwenyewe akiridhika na kurejea kwenye kiti chake, hali iliyosababisha Naibu Waziri mwenzake, Omar Mzee kumsaidia kujibu swali hilo.

Wakati akiuliza swali la nyongeza, mbunge huyo alitaka kujua kwa nini kodi za mishahara ya wafanyakazi wa Jamhuri ya Muungano walioko visiwani humo zisiwanufaishe wananchi wa huko.

Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alisema kuwa wafanyakazi wamekuwa wakikatwa kodi kutoka katika mishahara yao ili kuchangia huduma za jamii na mambo mengine kwanini walioko Zanzibar wasikatwe na fedha zibaki huko kwa ajili ya Zanzibar.

Akijibu swali lililomshinda Sumari, Mzee alisema pale ambapo mishahara inakokotolewa ndipo ambapo kodi inakatwa na kuwa mishahara aliyoizungumzia mbunge huyo huwa inakokotolewa Tanzania Bara.

Awali akijibu swali la msingi la Khamis Sumari alisema kodi ya mapato ni kodi ya muungano na hutozwa kwa utaratibu wa zuio kama ilivyoainishwa katika sheria ya kodi ya mapato.

Alisema utaratibu unampa mwajiri kukata kodi mahali ambapo hati ya kutayarisha mshahara wa mfanyakazi huandaliwa.

Alibainisha kuwa hati ya malipo hutayarishwa Bara, kodi ya mapato hukatwa Bara na kuingizwa katika mfuko mkuu wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano na kama hati hiyo ya malipo hutayarishwa Zanzibar, kodi ya makato hukatwa Zanzibar na huingizwa katika mfuko Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment