Tuesday, February 16, 2010

MSETO WAWATESA WAPINZANI ZANZIBAR

Chama cha Wakulima Zanzibar (AFP) kimesema wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Wananchi (CUF), walifanya makosa kupitisha hoja binafsi ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, inayovitenga vyama vigine vya siasa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo-Zanzibar) jana, Mwenyekiti wa AFP, Soud Said Soud alisema chama chake kinaunga mkono kuwepo kwa serikali hiyo kwa sababu ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya kisiasa ya Zanzibar.

Hata hivyo alisema muundo wake uliopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi haufai, na serikali lazima isitishe utekelezaji wake hadi hapo marekebisho yatakapofanyika ikiwemo kuvipa nafasi vyama vingine kushiriki kuunda serikali hiyo.

Hata hivyo, alisema kwamba viongozi Zanzibar wasiwe wepesi wa kusahau historia ya kisiasa ya Zanzibar kwa sababu mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalifanyika baada ya Chama cha Afro Shirazi Party kuchoshwa na vitendo vilivyokuwa vikifanywa na vyama vya ZNP na ZPP, kutoshirikishwa katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Alisema tayari chama hicho kimewasilisha barua maalumu serikalini kuitaarifu kuwa kina nia ya kufungua kesi mahakamani, kama ushauri wao hautozingatiwa ndani ya siku 20.


No comments:

Post a Comment