Wednesday, February 10, 2010

AJUZA WA MIAKA 80 ABAKWA BAGAMOYO

Ajuza wa miaka 80, mkazi wa kitongoji cha Kiwangwa wilayani Bagamoyo amebakwa na kijana mwenye umri wa miaka 35 na kusababishiwa majeraha makali katika sehemu zake za siri.


Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia jana na kwamba kijana aliyehusika na tukio hilo (jina linahifadhiwa), lakini ni mkulima wa Kiwangwa wilayani humu.


Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma alidhibitisha tukio hilo na kusema kuwa bibi kizee huyo alibakwa wakati akiwa amelala nyumbani kwake ambapo mtuhumiwa alitumia mbinu ya kuvunja mlango usiku huo na kuingia katika chumba cha ajuza huyo kisha kumbaka kwa nguvu.


Mwakyoma alisema tukio hilo linasikitisha na kutia aibu vijana kutokana na ukweli kwamba bibi huyo anaishi kwa shida na taabu nyingi.


"Inavyoonekana huyo jamaa, alikuwa anamvizia ajuza kwa muda mrefu na nadhani alikuwa akimfuatilia kwa karibu ili kujua mwenendo mzima,alipobaini analala mwenyewe ndipo alipotumia mbinu ya kumvizia muda huo na kuvunja mlango na hatimaye kumbaka hata imani za kishirikina zinaweza kuwa ni chanzo,"alisema Mwakyoma.


Alisema mlalamikaji anaishi mwenyewe kwenye nyumba hiyo na kwamba tayari mtuhumiwa alikamatwa na anaratajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara uchunguzi utakapokamilika, mlalamikaji anaendelea vizuri.


Katika tukio jingine Kamanda huyo wa Polisi Pwani alisema mkazi wa Kongowe wilayani Kibaha,(Jina linahifadhiwa) alikamatwa kwa kosa la kukutwa na meno ya tembo vipande vinne vyenye uzito wa kilogramu 15.1 vya thamani ya Sh 1.1milioni.


Tukio hilo lilitokea saa 8.00 mchana juzi katika eneo la shule ya msingi Kongowe na waliomkamata mtuhumiwa huyo ni maafisa wa maliasili wa kituo cha Kongowe kwa ushirikiano na askari polisi na kwamba mzee huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

No comments:

Post a Comment