Tuesday, December 22, 2009

WAZANZIBARI TUMECHOKA NA MASWALI

Na mwandishi wa MZALENDO.NET

Utangulizi: Wengi wetu tushachoka na masuali, kwa muda wa miaka karibuni 50 sasa
wazanzibari tumekuwa tukijiuliza bila ya kupata majibu.Nami sitouliza zaidi ya hapo, naamini sasa ni wakati wa majibu. Japo hayatokuwa na ukamilifu,lakini yatatusaidia kutupatia muelekeo.Kwenye nia pana njia, inshallah M.Mungu atawalipa wale wote wanaodanganya na kuficha ukweli wa historia ya visiwa vyetu vya Zanzibar.Leo mzanzibari anazaliwa anakwenda skuli kusoma, badala yake anapotoshwa kwa makusudi. Kama tujuavyo kuwa mali ni fitna,ukiona vita au vurugu jua chako chaliwa kimagendo.Nenda Iraq,vita vingi watu waibiwa mafuta yao.Ukitoka hapo elekea Congo, vita havishi ujue madhahabu na almasi zaibiwa kwa njia za panya.

Ngwe ya muungano:Tukirudi visiwani Zanzibar, jee hii ni kweli kuwa vurugu zinazoendelea au zilizotokea nchini mwetu watu wanaiba nini?Suali gumu sitokuwa na majibu ya papo kwa hapo, lakini pengine na tujaribu kujiuliza ni kipi ambacho wenzetu hawa wa CCM Zanzibar kinachowapelekea kung’ang’ania mfumo wa muungano ambao unatuburuza wazanzibari na kutupotezea rasili mali zetu.Hili limekuja wazi kwenye suala la mafuta ya Zanzibar na ndipo CCM kwa CUF barazani waliamka.Wengine tukaanza kukuna vichwa na kutafuta panadoli za kutuliza
maumivu.

Tukarudi kwenye shina la tatizo, mkataba mbovu wa muungano.Zanzibar imeingizwa mkataba huu na hawa makada wa CCM ambao.Vyereje sasa wamekuwa mstari wa mbele kupiga kelele za mafuta.Walitutosa kwenye mkataba usio na maslahi kwetu bila ya ridhaa yetu.Sasa jee wanakiri kama mkataba wa muungano una makosa na unahitaji marekebisho?au hawakuona wakati mafuta na mengineyo zaidi ya yale 11 ambayo baba etu Mh.Karume alikubaliana na Nyerere.Au walipewa asilimia 10% ili mafuta yetu yaibiwe?Au wanapiga kelele kwa kuzitumia hisia zetu
kujitafutia umaarufu wa kisiasa?

Kama utapenda maoni yangu ambayo utafiti wake ni wa kubaka hapa na pale, muungano ni batili. Haukuwa na wala haujawahi kuwa na ridhaa yetu.Kila mtu ana haki ya kuwa na mawazo tofauti kwenye suala hili, mimi napenda kutumia mawazo yangu kama kijana na kubatilisha muungano na wewe unaweza kufikiria utakavyo na kama utakuja na ushahidi wa kunionesha kama vyombo vya wazanzibari vilipitisha muungano, basi naweza kubadilisha mawazo na msimamo wangu. Hadi leo bunge linakimbia kutoa mkataba huo hadharani kwa sababu wazijuazo wao pekee.Iwavyo na iwe, muungano upo. Ukitaka usitake,upende usipende muungano upo.

Hoja ya msingi sio vipi tumeingia kwenye muungano, bali ni vipi tunafaidika na muungano huu na kama hauna faida vipi kujinasua.Huu ndio mjadala ambao kila kiumbe ambae anaishi Tanganyika au Zanzibar anatakiwa kutafakari.Pengine serekali ya Muungano iko siku itatusikia kelele zetu na kufanya utafiti mzima ili tujue kwa kina nani atasaga mawe pindipo utavunjika.

Maoni yangu binafsi ni yale yale ya umoja ni nguvu, lakini ili Zanzibar inufaike na muungano na Tanganyika ni kwa njia ya shirikisho la nchi za Afrika Mashariki na si vyenginevyo.Zanzibar na Tanganyika ni majirani na hilo haliondoki, vyovyote iwavyo ni kweli umoja ni nguvu.Lakini
tukumbuke utaifa wetu wa kizanzibari ndio majivuno yetu, na katu asilani wazanzibari hatutokubali kuvaa vikofia vya kitanzania.Kwa maana nyengine wazanzibari ni kama taifa jengine hatuko tayari kupoteza utaifa wetu, mila na utamaduni wetu!Tunataka bendera ya Zanzibar ipepee milele! Hakuna mjadala CCM Zanzibar ina uongozi tata katika kusimamia maslahi yetu.Au ndio hoja ile ya mali,na ndio vurugu hazishi Zanzibar.Isijekuwa wazanzibari
tunaibiwa na wenyewe tumetulia kama tuliomwagiwa maji.

Uzalendo wa Tanganyika:Kuna kitu cha kizalendo ambacho mara nyingi nimekuwa nikiganda bila majibu, hapa ni suala la uzalendo. Unajua sijaona sehemu duniani ambayo wananchi wake hawana uzalendo na majisifu kuhusiana na utaifa wao, na hao basi ni watanganyika.Sijawahi kumuona mtanganyika akijisifu kuwa yeye ni mtanganyika, hii ni tofauti na upande wa Zanzibar.Wazanzibari wao kokote unapo wakuta wanataka kujitambulisha kwa majivuno kama ni wazanzibari, na sio watanzania. Pengine hiki ndio chanzo cha matatizo yote ya kuwa Tanganyika na wananchi wake hawana tatizo lolote kwao kukosa au kupoteza utaifa wao.Manaake mara nyingi tumekuwa tukisikia kelele za wazanzibari kukimbia kupoteza serekali yao ya mapinduzi, ambayo kwa sasa japo ipo kama pambo bila ya mamlaka yoyote.

Hapa natumia neno “pambo” kwa kuwa haina madaraka hata ya kumuuwa mbu nchini
mwake bila ya ruhusa kutoka Dodoma.Hapa utashangaa kuona kuwa CCM Zanzibar wamenyamaza kimya, wanaguna wakiwa vichochoroni kuwa rais wao hana mamlaka yoyote na wala hatambuliki duniani.Hapa tusikimbie hoja za msingi, ni uongozi mama wa CCM ndio uliongia kwenye mkataba mbovu wa muungano na ndio wao waliopunguza mamlaka ya Zanzibar kutoka 11 hadi 22.

Hapa leo tukiwaona wawakilishi wa chama tawala wakililia na mafuta, tuwaulize wabunge wenzao waliopitisha kuwa mafuta yetu yagawiwe sawa bin sawa na huku wakigonga
madeski yao kuwa wamefurahia posho watokapo bungeni! Nia na madhumuni ya sera za CCM ni kuvimeza visiwa bila ya kuchakuwa.Huu ndio ukweli mzanzibari, na sio kama tunatia kasumba.Miongoni mwa sera za CCM ni serekali moja, lakini hurusha vumbi la macho kwa kutuambia ati serekali 2 kuelekea moja.Mie binafsi yangu ningelisema sera haswa ni serekali moja, lakini hawa watu wako mawindoni.Mtu anapowinda, hakurupuki na kuanza kutumia
silaha zake.

Kwanza hutumia mbinu za kunyatia na kusubiria hadi muda muafaka unapowasili ndio huanza mashambulizi ili kupata kufanya mauaji na kupata kitoweo.Kwa hiyo Tanganyika mawindoni, na kusubiria ili waimeze Zanzibar kwa mkupuo mmoja!Hii ndio maana ya kuanza mkataba mdogo wa vitu 11, halafu kuongeza hadi 22 na mwishowe ni kufuta serekali ya Zanzibar na kubakia serekali ya Tanganyika ikitawala eneo la Zanzibar kama sehemu yake tokea awali. Ni wapi wameshafanikiwa hadi hapa tulipo kwa mfumo huu tulionao?Tukizingatia serekali yaTanganyika imevaa koti la Tanzania,na kuviburuza visiwa vyetu!

Woga ni udhaifu:Si lengo langu kuingia kwenye siasa, mimi binafsi yangu sifati mlengo wowote.Sababu yangu ya msingi ni kupinga muungano, nahakuna chama kinachounga mkono sera yangu.Lakini inauma kumuona kiongozi wetu akisema Zanzibari ni nchi ukiwa ndani ya Zanzibar, na ukitoka nje basi si nchi.Inaniuma kumuona mzanzibari anasherehekea shangwe za siasa huku nchi yake inamezwa na Tanganyika kwa kisingizio cha muungano.

Haki ya kuunga mkono chama fulani ni ya msingi kwa kila mzanzibari, lakini tungeliomba tafadhalini mukatafakari sera za vyama hivyo kabla ya kuviunga mkono.CCM na hii sera ya serekali 2 kuelekea moja ni dhahir kuwa si njema kwa visiwa vyetu vya Zanzibar.Na kila mzanzibari hana budi kusimama kidete kuwa ifutwe, na kama haifutiki basi wazanzibari musikiunge mkono chama hicho!

Tumekuwa tukiona CCM Bara wakipiga kelele za ufisadi hadharani, ni kipi CCM wetu wa Zanzibar wanachoogopa kusema sera hii ya serekali moja haina maslahi kwa Zanzibar?Unaponyamaza kimya manaake umeikubali, waingereza wamesema “big silence means YES”.Sasa CCM wa Zanzibar tunataka mutoke hadharani kupinga sera hii kwa maslahi ya Zanzibar.Sasa siku ikifika na kikao cha NEC kikisema kinatekeleza sera hii, mutasema nini?Niliahidi kuwa huu ni muda wa majibu, sio masuali kwa hivyo hapa jibu letu la kuwa hawa CCM Zanzibar walionyamazia kimya manaake wanaifurahia na kuiunga mkono!Wasitupumbaze
pale wanaposema ati hakuna CCM Zanzibar atakae kubali serekali moja, hiyo ni danganya toto tuu.

Nishawahi kumsikia kada wa CCM kutoka Zanzibar akisema kuwa hakuna CCM wa Zanzibar atakae ikubali sera hii, sasa kwanini hawaikemei?Kama hawakemei basi wanafaidika kwa aina moja au nyengine.Vyovyote iwavyo wana sababu zao za msingi za ukimya huu, cha msingi ni kwetu wazanzibari kufanya maamuzi kuwa sasa tumechoka na ukimya na woga usiokuwa na misingi yoyote.Huu sio muda wa kukaa na kutishana, muda ushafika wa kila mtu kutoa maoni yake kwa uwazi kabisa na wote tukajua kila mmoja wetu anachokitetea kama kina maslahi na visiwa vyetu ili tukiunge mkono au tukikatae.

Misho:Matatizo ya Zanzibar na suluhisho zake ziko mikononi mwa wazanzibari wenyewe, na wewe kama mwananchi una uwezo wa kutafakari sera ya kila chama kabla ya kukiunga mkono.Kama utahitaji mawazo yangu, basi Zanzibar tunahitaji uongozi mwengine ambao utakuja kurekebisha na kujadili masuali mazito tuliyonayo.

Tusijidanganye ati Mh.Kikwete anajadili kero za muungano, kipindi cha mwanzo kimekwisha na hana alilofanya badala ya kumtuma Mh.Pinda kututonesha vidonda vyetu.Anakimbia hoja za msingi,kwa kuunda kamati nje ya bunge.Hapa anatengeneza kero nyengine na kukiuka taratibu za utawala bora.Bunge ndio linatuwakilisha sisi wananchi na sio vijikamati,hivi kweli hivi vikamati vinaweza kutetea maslahi yetu wazanzibari? Kheri ndugu yangu ukaamka kutoka katika usingizi mzito wa CUF-CCM na ukasimama kidete kutetea maslahi ya Zanzibar.Kumbuka kuwa sisi tutaondoka duniani, na vizazi vyetu vitakuja kuturithi kile tulichowaachia.Uko tayari kuwaona wanao wakitanga njia bila ya kuwa na kwao?

No comments:

Post a Comment