Sunday, December 27, 2009
MNIGERIA ATAKA KURIPUA NDEGE MAREKANI
Umar Farouk Abdul Mutallab kijana wa Kinigeria mwenye umri wa miaka 23 ambaye alitunukiwa shahada ya uhandisi katika chuo kikuu cha University College of London mwaka jana, amesababisha mtafaruku katika safari za anga baada ya kujaribu kujiripua kwenye ndege yenye abiria 278 na wahudumu 11 iliyokuwa ikielekea Marekani ikitokea Uholanzi.
Sheria kali zimewekwa kufuatia tukio hilo lililotokea siku ya krismasi ambapo Umar alijaribu kujiripua ndani ya ndege ya Northwest Airlines zikiwa zimebaki dakika 20 kabla ya ndege hiyo kutua kwenye uwanja wa ndege wa Detroit.
Umar aliungua moto robo tatu ya mwili wake kutokana na mlipuko uliotokana na kifaa chake alichokuwa amekificha ndani ya suruali yake.
Taarifa zilizotolewa zilisema kwa Umar kabla ya kufanya jaribio lake hilo la kujilipua, alienda kwenye choo cha ndege hiyo ambapo alitumia dakika nyingi na aliporudi alisema anasumbuliwa na matatizo ya tumbo na kuomba blanketi ajifunike.
Akiwa ndani ya blanketi lake, alitengeneza bomu lake kwa kuunganisha kemikali alizokuwa amezibeba na kusababisha mlipuko ulioambatana na moto.
Kabla hajatimiza azma yake ya kuseti bomu lake vizuri, abiria waliokuwa pembeni yake walimrukia na kumzuia asitimize azma yake.
Wahudumu wa ndege walifanikiwa kuuzima moto uliotokea kwenye ndege hiyo ambao uliiunguza suruali yake na kumuunguza mwenyewe robo tatu ya mwili wake.
Umar yuko chini ya ulinzi mkali katika hospitali aliyolazwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyopata kufuatia moto aliousababisha.
Umar inasemekana kuwa aliwaambia maafisa wa Marekani baada ya kukamatwa kuwa ana uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda na alipata mafunzo yake nchini Yemen.
Baba yake Umar ambaye ni tajiri maarufu nchini Nigeria inasemekana alishatoa taarifa kwenye ubalozi wa Marekani nchini Nigeria miezi sita iliyopita kuhusiana na siasa kali za mwanae dhidi ya Marekani.
Kufuatia tukio hilo, sheria kali zimewekwa kwa ndege zinazoenda Marekani ambapo abiria watatakiwa kutonyanyuka kwenye siti zao kwenda kokote ndani ya lisaa limoja kabla ya ndege kutua.
Pia abiria hawatapewa tena mablanketi ya kujifunika kwenye ndege zinazoenda Marekani wakati ndege zitakapokaribia kutua.
Mbali na hatua hizo, abiria pia watatakiwa kuwa na begi moja tu la mkononi na watalazimika kufanyiwa X-ray za vifaa vyovyote vya milipuko kwenye miili yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment