Monday, November 23, 2009

MAHUJAJI WANNE WAFARIKI KWA MAFUA YA NGURUWE

Mahujaji wanne waliokuwa nchini Saudi Arabia kuungana na mamilioni ya mahujaji toka nchi mbali mbali duniani kwaajili ya hija kubwa, wamefariki dunia kutokana na mafua ya nguruwe.

Mwanaume mmoja toka India, mwanamke mmoja toka Morocco na mwanaume mwingine toka Sudan wote wenye umri zaidi ya miaka 75 pamoja na msichana mwenye umri wa miaka 17 toka Nigeria wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa homa ya mafua ya nguruwe walioambukizwa wakati wa hija.

"Wote walikuwa na matatizo mbali mbali ya kiafya kabla ya kukumbwa na mafua ya nguruwe, msichana wa Kinigeria alikuwa na matatizo ya kifua", alisema msemaji wa wizara ya afya ya Saudia, Khaled al-Marghlani.

"Pia hakuna hata mmoja wao aliyepiga sindano ya chanjo ya ugonjwa wa mafua ya nguruwe", aliongeza msemaji huyo wa wizara ya afya.

Takribani waislamu milioni 2.5 wanatarajiwa kuhudhuria hija ya mwaka huu, ukiwa ni mkusanyiko mkubwa kuliko wote wa watu tangia ugonjwa wa mafua ya nguruwe ulipogunduliwa nchini Mexico mwezi aprili mwaka huu.

Watu 20 wamegundulika kuambukizwa mafua ya nguruwe tangia hija zilipoanza katika miji ya Makka na Madina na 12 kati yao walipatiwa matibabu na kutolewa hospitali wakati watu wanne bado wamelazwa hospitali.

Wataalamu wa masuala ya afya wamesema kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa katika kiwango kidogo sana kuliko ilivyohofiwa kutokana na tahadhari zilizochukuliwa.

Wataalamu wa afya 20,000 wamepelekwa kwenye miji ya Makka, Madina na Jeddah kuwa tayari tayari kupokea watu watakaoambukizwa ugonjwa huo huku hospitali zimewekwa mamia ya vitanda vya ziada.

Mawe yatakayotumika kuipiga alama ya shetani wakati wa hija, nayo yamewekwa madawa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Watu wenye magonjwa sugu, wazee sana, watoto na wanawake wenye mimba wametakiwa kuahirisha safari zao za hija mwaka huu.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO, watu 6750 wamefariki duniani kutokana na ugonjwa wa mafua ya nguruwe tangia ulipogunduliwa nchini Mexico na Marekani mwezi aprili mwaka huu.

Waislamu hutakiwa kuhudhuria ibada ya hija mara moja katika maisha yao iwapo watakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Sikukuu ya Idi itasherehekewa ijumaa wiki hii huku baadhi ya nchi zingine zikisherehekea jumamosi.

No comments:

Post a Comment