Saturday, November 21, 2009

AFUNGA NDOA NA BINTI YAKE KWA AJILI YA MAKARATASIMzee Jelili Adesanya mwenye umri wa miaka 54, mzaliwa wa Nigeria mwenye pasipoti ya Uingereza anafanyiwa uchunguzi baada ya kugundulika kuwa amefunga ndoa na binti yake wa kumzaa.

Mzee Jelili ambaye yupo nchini Uingereza tangia mwaka 1976 anatuhumiwa kufunga ndoa na binti yake Karimotu Adenike na kuishi naye kwa kuzuga kama mke wake ili aweze kupata "makaratasi" ya Uingereza.

Magazeti ya Uingereza yalitoa habari hii yakiambatanisha na picha ya harusi ya Jelili na binti yake wakiwa wameshikana mikono kama maharusi wa kweli.

Taarifa zilizotolewa na karibia magazeti yote ya Uingereza zilisema kwamba Jelili alifunga ndoa ya bomani na binti yake nchini Nigeria tarehe 29 mwezi mei mwaka 2007 na baada ya hapo aliomba viza ya miaka miwili ya ndoa kumwezesha "Mke wake" (binti yake) aishi Uingereza. Alipewa viza hiyo mwezi oktoba mwaka huo huo.

Baba na mwanae walikuwa wamepanga kuwa baada ya miaka miwili, binti yake atapata sheria za Uingereza za kumruhusu kuishi milele Uingereza na hivyo ataivunja ndoa yake na baba yake na kisha atafunga ndoa tena lakini safari hiyo itakuwa na mumewe wa kweli anayeishi Nigeria ambaye amezaa naye watoto wanne.

Mpango huo umeingia chachu baada ya mdaku mmoja asiyejulikana wa nchini Nigeria kuripoti ubalozini, wizarani mpaka kwa mawaziri kuwa mzee huyo amefunga ndoa na binti yake.

Taarifa zilisema kwamba wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza ilitaarifiwa suala hilo na mdaku huyo miaka miwili iliyopita lakini haikuchukua uamuzi wowote.

Mdaku huyo awali alituma barua ubalozi wa Uingereza nchini Nigeria akiwataarifu suala hilo akiambatanisha majina yao, anuani zao, namba za pasipoti zao mpaka picha ya harusi yao.

Baada ya kuona hamna hatua yoyote iliyochukuliwa, februari mosi mwaka huu mdaku huyo aliamua kuwatumia email waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza wa wakati huo, Jacqui Smith na mawaziri Vernon Coaker na Phil Woolas lakini mawaziri hao nao hawakuchukua hatua yoyote.

Taarifa zaidi zilisema kwamba Adenike alibadilisha umri wake kwenye pasipoti yake kwa kujiongezea miaka 10 zaidi ili kusiwe na tofauti kubwa ya umri kati yake na baba yake. Adenike hivi sasa ana umri wa kwenye miaka ya 30 na ushee.

Taarifa zaidi zilisema kwamba hata harusi yao iliyofanyika Nigeria ilifanyika kwa kuzuga kwa kukodisha wahudhuriaji wa harusi hiyo ili ionekane kama ya kweli.

Zengwe la ndoa yao limebumbuluka hivi sasa baada ya viza ya miaka miwili aliyopewa Adenike kuisha na akiwa kwenye hatu za mwisho za kuomba sheria ya kuishi Uingereza milele.

Jelili na binti yake wanafanyiwa uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na maafisa wa uhamiaji wa Uingereza wamesema kuwa ikithibitika kuwa tuhuma hizo ni za kweli basi Jelili na binti yake watapandishwa kizimbani na huenda wakatupwa jela kabla ya kurudishwa Nigeria." />

No comments:

Post a Comment