Umoja wa Wazalendo
“Na shikamaneni kwa Dini ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja,
wala msifarikiane…”.
Wazee wetu, Ndugu zetu,
Assalaam Alaaykum,
UMOJA, UHURU, UADILIFU
UMOJA NA MSHIKAMANO NDIO NGAO ZETU
Maneno haya ya hikma, “Umoja na Mshikamano ndio ngao zetu”, yamebainishwa tena hivi karibuni na Rais wa Zanzibari, Mhishimiwa Aman Abeid Aman. Yamesemwa, kuandikwa kwa khati kubwa na kuwekwa sehemu mbalimbali. Yamebainishwa kwa hali hii, ili daima sisi Wazanzibari tuzidi kuyazingatia na kuyafanyiakazi. Hapana shaka maneno haya ni kulingana na Maamrisho ya Mola wetu Mlezi, Subhaanahu wa Taáala anavyotwambia:
“Na shikamaneni kwa Dini ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane…”.
Umoja wa Wazalendo, unatoa shukrani za dhati kwa Mhishimiwa Rais Aman; na kuahidi kuyazingatia kwa kina kabisa, kuyathamini na kuyafanyiakazi maneno haya kila wakati. Hivi zaidi ni kutokana na imani ya Wazanzibari kwamba “Umoja na Mshikamano” ndio nyenzo kuu ya kuendeleza juhudi za kuitoa Nchi yetu, Zanzibar kutokana na makucha ya “mkoloni mvamizi; Tanganyika” na kuirejesha Dola Huru Kaamili ya Zanzibar kama ilivyokuwa siku ile ilipojiunga na Umoja wa Mataifa, Disemba kuminasita, 1963.
Umoja wa Wazalendo, unatambuwa vyema kuwa kila ukizidi kushamiri na kudhihiri Umoja na Mshikamano wa Kizanzibari, ndivyo mkoloni mvamizi; Tanganyika anavyozidisha mbinu zake ovu za kuwagombanisha Wazanzibari ili kuwafarikisha hivyo aendeleze kwa mbinu na nguvu utawala wake wa kikoloni juu ya Zanzibar. Umoja wa Wazalendo, unatambuwa vyema kuwa huu ukatili unaofanywa na majeshi ya mkoloni mvamizi, Tanganyika katika hiki kipindi cha kuelekea uchaguzi ni miongoni mwa mbinu hizo za kuwagombanisha na kuwafarikisha Wazanzibari. Lakinibasi, lazima atambue mkoloni mvamizi; Tanganyika kwamba zama za kuwagombanisha na kuwafarikisha Wazanzibari zimeshapitwa na wakati. Wazanzibari daima watasimama begakwabega katika juhudi za ukombozi wa Nchi yao, Zanzibar.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, Subhaanahu wa Taáala atujaalie kila kheri na atuepushe na kila shari; na atujaalie ufunguzi wa karibu, Aamyn.
Wa Billahi Tawfiiq
Umoja wa Wazalendo
Zanzibar, Ijumaa October 02, 2009
“…. وأمرهم شورى بينهم ……”.
“….., na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao,…..”.
No comments:
Post a Comment