Katika mkutano wa dharura mjini Brussels, Ubelgiji, viongozi wa mataifa 16 yanayotumia sarafu ya Euro, wameidhinisha mkopo wa kuikoa Ugiriki isifilisike. Hata hivyo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema kundi hilo la mataifa 16, litatoa ujumbe maalum kwa walunguzi, kwa kuanzishwa mfuko maalum wa dharura kwa azma ya kuzuia matatizo ya kideni katika mataifa mengine ya Ulaya.
Serikali ya Ugiriki imechukua jukumu la kubana matumizi yake kama njia ya kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ili iweze kupata mikopo ya dharura kutoka nchi za kanda ya euro na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.
Hata hivyo hatua hiyo ya serikali ya Ugiriki imepingwa vikali na raia nchini humo. Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou akizungumza huko mjini Brussels alisema sio nchi yake pekee ilio hatarini.
Nalo bunge la Ujerumani,wabunge wake wameidhinisha mswada wa sheria itakayotoa fursa ya kuipa mkopo Ugiriki. Rais Horst Köhler ametia saini mswada huo kuwa sheria. Kuambatana na makubaliano ya mkopo huo, Ujerumani itaipatia Ugiriki Euro bilioni 22.
Katika kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro, Ujerumani inatoa sehemu kubwa ya mkopo huo kwa sababu pia ni nchi iliyo na uchumi mkubwa kabisa katika kundi la mataifa 16 yanayotumia Euro.
.
No comments:
Post a Comment