Mashoga wa nchini Malawi ambao walifunga ndoa hivi karibuni nchini humo walinyimwa dhamana na kurudishwa jela wakisubiria hukumu ya kesi yao ya kufanya kitendo nje ya maadili ya jamii.
Steven Monjeza akiwa na mkewe Tiwonge Chimbalanga ambaye alikuwa amevaa nguo za kike gauni na kitenge alipofikishwa mahakamani walizomewa na kupigiwa kelele na mamia ya watu waliojiotokeza mahakamani wakati walipopigwa pingu na kupandishwa kwenye karandinga kurudishwa jela baada ya jaji kukataa kuwapa dhamana.
Monjeza na Tiwonge wataendelea kuwa jela mpaka wiki ijayo wakati kesi yao itakapoanza kusikilizwa na huenda wakatupwa jela miaka 14 iwapo watapatikana na hatia.
Akiwanyima dhamana jaji Nyakwawa Usiwa-Usiwa alisema kuwa ni bora wakaendelea kukaa mahabusu ambako ni salama kuliko kukaa uraiani ambako kuna watu wengi wenye hasira kufuatia uamuzi wao wa kuoana.
"Anti Tiwonge, Anti Tiwonge", walipiga kelele mamia ya watu waliojitokeza mahakamani kushuhudia ndoa ya kwanza ya mwanaume kwa mwanaume nchini Malawi.
"Oh tunarudishwa tena kwenye jela ya Chichiri, hali ni ngumu sana kwenye jela ile", alilalama Monjeza ambaye alidai anafikiria kumtosa mkewe kufuatia hasira kali za wananchi.
Wakati huo huo wanaharakati wa kutetea haki za mashoga duniani wameijia juu serikali ya Malawi kufuatia taarifa kuwa Monjeza na Tiwonge walikaguliwa sehemu zao za siri na maafisa wa Malawi ili kujua kama wameishafanya mapenzi kinyume na maumbile.
Awali mwendesha mashtaka wa serikali alisema kuwa Monjeza na Tiwonge wamekuwa wakiishi pamoja kama mume na mke tangia mwezi agosti mwaka jana hivyo alitaka wapelekwe hospitali kupimwa kama wameishajamiiana kinyume na maumbile.
Monjeza mwenye umri wa miaka 26 na Tiwonge mwenye umri wa miaka 20 wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kufanya vitendo ambavyo si vya asili kwa wanaume na kwa mujibu wa sheria za Malawi adhabu yake ni miaka 14 jela.
No comments:
Post a Comment