Sunday, July 25, 2010

IJTIMAI ZANZIBAR - 2010

Salma Said,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Amani Abeid Karume ametoa wito kwa Waislamu na wananchi wote wa Zanzibar kuunga mkono kura ya maoni kwa lengo la kuendeleza amani, mshikamano na kutofarikiana miongoni mwao kama Uislamu unavyosisitiza.

Rais Karume aliyasema hayo leo huko katika Msikiti wa Markaz Kuu Fuoni Migombani katika horuba yake aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Ijtmai ya 17 ya Kimataifa na kusisitiza kuwa zoezi la kura ya maoni linalotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu ni ishara tosha ya kujenga umoja na mshikamano na hakuna sababu ya kukataa kwani sio jambo baya.

Katika hotuba yake hiyo, Alhaj Karume alisema kuwa Umoja wa Wazanzibari utafungua ukurasa mpya na kueleza kuwa dini ya Kiislamu imekuwa ikisisistiza amani na mshikamano miongoni mwa Waislamu hatua ambayo imefikiwa kwa kiasi kikubwa hapa Zanzibar hivi sasa.

Alhaj Karume alisema kuwa ni kawaida kila inapofika katika kipindi kama hichi Zanzibar kugubikwa na shughuli za kisiasa ambazo wakati mwengine hotukezea mambo ambayo hayana maslahi kwa wananchi lakini katika kipindi hichi mafanikio makubwa yamepatikana.

Alieleza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na maridhiano yaliofanyika kati yake na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuangalia mustakbali wa nchi na wananchi wake hatua ambayo imeweza kuungwa mkono na wananchi walio wengi.

Rais Karume alieleza kuwa anafarajika kuona na kusikia Waislamu nchini pamoja na wananchi kwa jumla wakiunga mkono maridhiano hayo na kusisitiza kuwa sifa na hongera anazopewa kwa kuweza kuifikisha Zanzibar katika medani na amani na utulivu si zake pekee bali ni za wananchi wote wa Zanzibar.

Alhaj Karume alisisitiza kuwa umoja, amani na utulivu ndio msingi wa maendeleo na jambo hilo sio jipya kwa Zanzibar na kueleza kuwa umoja ni miongoni mwa Sera za Chama Cha Mapinduzi..

Rais Karume alitoa shukrani kwa maandalizi ya Ijtmai hiyo ya 17 sanjari na hatua nzuri za ujenzi zilizofikiwa na kuahidi kutoa ushirikiano wake kwa kuahidi changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi ikiwemo ujenzi wa barabara inayoelekea Markaz hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami, kuwapatia usafiri na kuwatafutia viongozi wa Markaz nafasi za Hijja.

Aidha, Rais Karume alieleza kuwa lengo la serikali la kujengwa Chuo Kikuu cha Kiislamu lipo pale pale na juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha linafanikiwa na kuwaondosha hofu wale wanaodhani kuwa vyuo vya Kiislamu huwa vinatoa elimu ya msimamo mkali.

Nao Waislamu nchini wameleleza kuridhishwa na maridhiano yaliofanyika kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj. Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na kueleza kuwa hatua hiyo ni maamrisho ya Allah ya kuimarisha umoja na kutofarikiana.

Akisoma hotuba fupi ya makaribisho, Mwenyekiti wa Jumuiya za Markazi Kuu ya Fuoni Amir Ali Khamis alisema kuwa leo ni siku ya faraja kubwa na furaha isiyokifani kwa Waislamu na wananchi wa Zanzibar wapenda Amani na Utulivu na salama nchini.

Amir Khamis alitoa wito kwa Waislamu wote na wananchi wote kwa ujumla kuunga mkono kwa dhati kabisa maridhiano hayo kwa faida ya Waislamu na Wazanzibar wote..
Alieleza kuwa Wazanzibari na Waislamu wa Zanzibar wamechoka na hasama na mabalaa yasiyokwisha kila panapoingia uchaguzi nchini “Tunatoa wito kwa Wazanzibari wote kuyapokea maridhiano haya kwa mikono miwili”,alisema Amir.

Nae Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akitoa salamu zake kwa Waislamu waliohudhuria katika Ijtmai hiyo alieleza kuwa ni faraja kuwa kwa wananchi wa Zanzibar chini ya uongozi wa Alhj Karume wanakaa pamoja na kushirikiana kama dini inavyotaka.

Alisema kuwa hatua hiyo inaonesha dalili za umoja ziko wazi wazi kabiza na kusisitiza umuhimu wa kura ya maoni mwishoni mwa mwezi huu kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu kwa kuunga mkono kwa kukubali umoja huo.

Akitoa hotuba ya Sala ya Ijumaa. Sheikh Othman Maalim alieleza kuwa maridhiano ya viongozi hao yanatokana na maarisho ya Mwenyezi Muungu ya kuwataka waumini kushikamana na kutofarikiana.

Maelfu ya Waumini kike kwa kiume wadogo kwa wakubwa, Masheikh na Maulamaa kutoka nchi mbali mbali zikiwemo za Afrika pamoja wa Waumini wenyeji wa Unguja na Pemba na Mikoa ya Tanzania Bara wamehudhuria katika Ijtmai hiyo ya siku tatu.

1 comment:

  1. Mungu awape kheri walioandaa jitimai hii na inshallah malengo yatafikiwa.

    ReplyDelete