Wednesday, July 21, 2010

Ng’o sitopiga Hapana

Na. B.OlE

Naikumbuka Zanzibar nzuri ambayo imenilea, kunitunza kwa utulivu na amani. Maumbile mazuri ambayo macho yangu yalipofungua kutoka kwa mama mzazi yalinilaki na kunipongeza huku yakanikaribisha kwa bashasha na furaha nyingi.

Mazingira yenye harufu ya manukato yenye kuleta kila ainaya furaha na faraja. Zanzibar iliokuwa njema, amani, utulivu, upendo na ukarimu.

Zanzibar iliokuwa na watu wapole, wasomi, wenye mapenzi, haiba na furaha na bashasha wakati wote.

Zanzibar ilioungana huku wazee wakiwa wamebarizi kwenye sehemu zao wakiangalia vijana wao wakicheza kwa mbwembwe na furaha tele.

Zanzibar ambayo ugomvi, ubaguzi, ilikuwa ni mwiko na sumu kali miongoni mwa jamii.

Zanzibar ambayo bahari yake ilishuhudia majahazi na mitumbwi ikipishana kutoka kisiwa kimoja kwenda chengine kwa nyimbo na hoi hoi huku watu wakufurahia udugu pamoja na usahiba wao.

Zanzibar ambayo upepo wa pwani ulitawala kuleta hali nyororo yenye kukidhi haja ya viumbe huku ndege na wao wakiimba kwa furaha kufurahia Amani ya visiwa vyetu.

Zanzibar ambayo hata misitu haikurudi nyuma kuashiria manyunyu na rasha rasha za mvua za miongo za hapa na pale.

Zanzibar ambayo mbara mwezi ilimwilika huku watoto wakicheza kinyuli nyuli nyulika mwanangu mwana jumbe kavaa nguo mbili ya tatu kajibandika…….

Zanzibar ambayo matunda na vyakula mbali mbali yalioteshwa na kuwafanya watu kuwa na siha na furaha ya maisha yao.

Maumbile haya mazuri na yenye kuvutia machoni mwa kila mtu kwa tabasamu yaliniahidi kunitunza na kunipa kila aina ya maisha bora na ya furaha kabisa.

Najiuuliza haya yote yameenda wapi, mbona nimekuwa mkiwa ? Mama yangu Zanzibar amekuwa Mgonjwa na mimi mtoto sina furaha wala bashasha.

Sitosahau ihsani na fadhila ya nchi yangu ndio maana nikasema Ng’o sitopiga HAPANA kura ya maoni.

SABABU ZANGU MAALUM:-

1.Kusema Hapana ni kuisaliti nchi yangu, mama alonilea.

2.Ni kuitakia mabaya na kutoijali nchi ilionilea kwa mapenzi makubwa.

3. Nitakuwa nimechangia kupoteza ile hidaya muhimu kwa visiwa vyetu , yaani utulivu na amani.

4.Nitakuwa nimeshiriki kikamilifu kuendeleza chuki, uhasama na ugomvi wa wananchi wenzangu bila faida yeyote ile.

5. Nachelea kuja kuulizwa siku ya malipo juu ya mchango wangu wa kusaidia machafuko Zanzibar, sitokuwa na jibu siku hiyo.

6. Kumsaliti mlezi alienipokea kwa mikono miwili ni kosa kubwa kiasi ambacho nitatakuja kustahiki adhabu kali hapo baadae na laana ya mola inaweza kinishukia.

7.Kuwapinga walio wengi wanaoitakia Zanzibar mema na maslahi kwa wananchi wote ni kitendo kisichokubalika katika jamii ya wastaarabu.

8.Kwenda kinyume na maamrisho ya dini yetu yenye kuhimiza amani na upendo miongoni mwetu ni kosa kubwa.

9.Kuwanyima fursa muhimu kwa Wazanzibar kuondosha tofauti zao za siasa za chuki zilizodumu kwa muda mrefu sasa ni jambo lisilokubadilika abadan.

10.Kutowatakia mema kwa kizazi kipya na kuwarithisha chuki na uhasama kwa watoto wetu sio jambo la kufurahia.

11.Kuwapa nguvu wale wote wanaopinga umoja na ushirikiano miongoni mwa Wazanzibar sio busara na maadili mazuri.

12. Kufurahia kila baada ya miaka mitano kuona Wazanzibar wakiteseka na kudhalilishwa bila sababu na hatimae kuuwana ni kujidhalisha kwa nafsi na hukumu yake itakuwa nzito.

13. Kutesana wenyewe kwa wenyewe wakati sote ni watu wa asili moja ni jambo la kuhuzunisha sana.

14.Kufurahia kuwaona wengine wakibaguliwa kwa rangi,kabila na sehemu wanazotoka jambo ambalo hata Mola wetu halifurahii, mimi kama kiumbe sitaki niwe nimeshiriki kwa hilo.

15.Kutengana na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa letu ni kwanyima fursa wengine hasa kizazi kipya.

16. Kuleta migawanyiko ndani ya jamii na kuwafanya wengine waonekane wana haki zaidi juu wenzao jambo ambalo litapelekea mgawanyiko na mifarakano ndani ya jamii.

17.Kukaribisha na kuwafanya watu wachache wasimame juu ya sheria huku walio wengi wakionewa na sheria hizo hizo haikubaliki.

18. Kuwafanya wachache wafaidi matunda ya nchi yetu huku walio wengi wakipata shida na kuteseka na familia zao ni uchoyo mbaya.

19.Kupoteza muelekeo wa Dola yetu ya Zanzibar na kupoteza kila kilicho chetu, na hatimae kuwa ni watu tusiokuwa na kwetu, hili halikubaliki.

20.Kukaribisha mabaya na kuunda misingi ya chuki na fitina zisizo kwisha na kugawa matabaka miongoni mwetu, sitoridhia.

21.Kuwaunga mkono wale vibaraka, mafisadi, wahafidhina,wanafiq wasioitakia mema Zanzibar na Wananchi wake, ni kutoipenda nchi yangu.

KURA yangu sitopiga Hapana ng’o, wewe jee?

No comments:

Post a Comment